UN: Yatoa wito kupelekwa kikosi cha kimataifa nchini Haiti
17 Agosti 2023Guterres amerudia wito huo katika barua aliyoandika kwa baraza la usalama, ambapo ameshauri kwamba kikosi hicho kiwe cha polisi na wanajeshi.
Guterres na waziri mkuu wa Haiti Ariel Henry wamekuwa wanasisitiza wito huo kwa miezi kadhaa juu ya kupelekwa kikosi hicho nchini Haiti inayoendelea kuzama kwenye migogoro ya kisiasa na ukosefu wa usalama.
Mpaka sasa nchi nyingi zimekuwa zinasuasua kuchukua hatua hiyo lakini mwishoni mwa mwezi uliopita, Kenya ilitangaza kuwa tayari kuongoza kikosi cha polisi cha kimataifa kwa lengo la kuingilia kati nchini Haiti pamoja na kutoa mafunzo kuwasaidia polisi wa nchi hiyo.
Soma pia:Maelfu ya watu waukimbia mji mkuu wa Haiti unaokumbwa na machafuko ya magenge
Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameliunga mkono tangazo la Kenya. Hata hivyo kupelekwa wanajeshi na polisi wa kimataifa nchini Haiti kunahitaji ridhaa ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Magenge yanayotumia nguvu yanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu, Port-au-Prince na vitendo vya matumizi ya mabavu, vimekithiri ikiwa pamoja na utekaji nyara, ubakaji na unyanga’nyi.