1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaweka mkakati wa kutekeleza muafaka wa tabianchi

Caro Robi
19 Novemba 2016

Karibu mataifa 200 yamekubaliana kutengeneza ndani ya kipindi cha miaka miwili sheria za kuutekeleza mkataba wa kihistoria wa kimataifa uliotiwa saini mwaka wa 2015 ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

https://p.dw.com/p/2SvuW
Marokko Klimakonferenz in Marraesch
Picha: Flickr/COP22

Kwa kuonyesha dhamira yao ya kuyaweka Makubaliano ya Paris kwenye mkondo sahihi, nchi hizo zimesema orodha ya sheria itakamilishwa ifikapo Desemba 2018. Muafaka huo uliofikiwa na wajumbe wa Umoja wa Mataifa unakamilisha wiki mbili za mazungumzo mjini Marrakesh, Morocco.

Wajumbe pia walikubali katika waraka huo kukutana tena mwaka wa 2017 ili "kutathmini hatua zilizopigwa". Sheria hizo za mwongozo zitasaidia kuweka wazi maelezo mengi yaliyowachwa katika njia isiyoeleweka katika Mkataba wa Paris kaam vile namna nchi zitatafutulia ahadi zao za kitaifa kudhibiti uzalishaji wa gesi chafu na namna zitakavyoripoti maendeleo yao.

Nakala ya mwisho ya waraka uliokubaliwa Ijumaa pia ulizitaka nchi tajiri kiuchumi kuahidi kutekeleza lengo la kutoa dola bilioni 100 za ufadhili wa kila mwaka kwa mataifa yanayostawi ifikapo mwaka wa 2020. Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Morocco Salaheddine Mezouar alisema katika mkutano huo "tutaendelea kwenye mkondo huo".

Waziri wa Mambo ya nje wa Morocco Salaheddine Mezouar
Waziri wa Mambo ya nje wa Morocco Salaheddine MezouarPicha: Getty Images/AFP/F. Sienna

Ombi kwa Trump

Mezouar pia alitoa wito kwa Rais mteule wa Marekani Donald Trump kujiunga na mataifamengine katika dhamira zao za kupunguza uzalishaji wa gesi chafu. Trump ametoa kauli zinazopinga Mkataba wa Paris na ametishia kuutupilia mbali mkataba huo.

Aidha alisema mabadiliko ya tabia nchi ni utapeli ambao ulibuniwa na Wachina. Rais huyo mteule pia ameahidi kuimarisha uzalishaji nishati ya mafuta, gesi na mkaa dhidi ya vyanzo vya nishati mbadala na kutishia kuzuia fedha za mlipa kodi wa Marekani kutumika katika mipango ya Umoja wa Mataifa kuhusu tabia nchi.

Utekelezaji kamili

Serikali zilizokutana nchini Morocco zilisisitiza dhamira yao ya kutekeleza muafaka wa kimataifa wa mabadiliko ya tabia nchi. "Azimio la utekelezaji la Marrakesh " lilitoa ombi la kuwapo "dhamira ya hali ya juu ya kisiasa" kupambana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na "utekelezaji kamili wa Mkataba wa Paris”.

Ijapokuwa muda wa mwisho wa miaka miwili uliowekwa kwa ajili ya kutengeneza sheria za mwongozo wa Mkataba wa Paris huenda ukaonekana kuwa mrefu, ilichukua miaka minne kufikia sheria za kina kwa ajili ya Mkataba wa Kyoto wa mwaka wa 1997. Muafaka huo ulizihitaji nchi zilizostawi kiviwanda kupunguza uzalishaji wa gesi chafu, lakini Makubaliano ya Paris yanahitaji hatua za kujitolea kutoka mataifa yote.

Mkataba wa Paris uliidhinishwa kuwa sheria ya kimataifa mnamo Novemba 4 lakini utaanza kutekelezwa mwaka wa 2020. Mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utaandaliwa mwaka ujao mjini Bonn, Ujerumani

Mwandishi: Caro Robi/ rs/kl (AFP, dpa, Reuters
Mhariri: Bruce Amani