1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina milioni moja wapo katika kitisho cha njaa Gaza

5 Juni 2024

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa zaidi ya Wapalestina milioni 1 wa Ukanda wa Gaza wanaweza kukabiliwa na kiwango cha juu zaidi cha njaa ifikapo katikati ya mwezi ujao iwapo vita vitaendelea katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4ggQe
Kambi ya Wakimbizi ya Jabalia Ukanda wa Gaza | Watu hupanga mstari kutafuta maji
Watu wa Gaza wakisubiri maji katika uwanja wa shule iliyoharibiwa inayotumika kuwahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Juni 3, 2024.Picha: Omar Al Qatta/AFP/Getty Images

Katika ripoti ya pamoja iliyotolewa leo, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo, FAO, yamesema kwamba njaa inazidi kwa sababu ya vikwazo vya ufikiaji wa msaada wa kibinadamu katika eneo hilo pamoja na kuporomoka kwa mfumo wa chakula katika muda wa takribani miezi minane ya vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas. Ripoti hiyo imeongeza kuwa kwa kukosekana kwa usitishaji wa uhasama na ufikiaji wa eneo hilo, athari ya vifo na maisha ya Wapalestina sasa na katika vizazi vijavyo, zitaongezeka kila siku, hata kama njaa itaepukwa kwa muda mfupi.