UNCTAD yabaini kuwa sera za biashara huria zimeshindikana
17 Julai 2009Sera za biashara huria zimeshindikana, hivyo biashara huria ni bora ikasitishwa. Hayo ni baadhi ya matokeo na mapendekezo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, (UNCTAD), kwa ajili ya nchi masikini, ambazo nyingi za nchi hizo ni za Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Julai 16, mwaka huu na UNCTAD, katika nchi zinazoendelea, soko halijafanikiwa kuzalisha kwa pamoja. Umoja wa Mataifa kwa sasa unazizungumzia nchi 49 kama nchi zinazoendelea, 33 kati ya hizo ziko katika Bara la Afrika.
Mabadiliko makubwa yanahitajika katika sera za uchumi, kilimo na viwanda. Baada ya miongo kadhaa ya kupunguzwa bajeti, taifa lazima litumie fedha zake tena. Dokta Charles Gore, mwanauchumi wa juu wa UNCTAD, anasema sera za masuala ya fedha zilikuwa zikipewa kipaumbele miaka ya nyuma, lakini sera za hazina ya serikali ndizo zinachukua jukumu kubwa kwa sasa.
Nchi zinatakiwa zitekeleze kwa upana zaidi sera za hazina za serikali, mapato ya nchi kuwekeza katika sekta ya uzalishaji kama vile kilimo, miundombinu, afya na elimu. Kilimo ni sekta nyingine muhimu. Usalama wa chakula ni tatizo kubwa katika nchi zinazoendelea. Gore, anasema kuna haja ya kuongeza uzalishaji wa kilimo, siyo tu kwa kuwaangalia wakulima, lakini pia kwa kuboresha mfumo wa kilimo na kuliangalia zaidi suala la kufanya utafiti.
Nchi zinazoendelea katika Bara la Asia, hasa Bangladesh, hazikuathiriwa vibaya na msukosuko wa kiuchumi duniani, kwa sababu hawategemei sana uuzaji wa bidhaa nje na zina sekta imara ya viwanda. Taifa linahitaji kugeukia maendeleo ya utawala bora kulingana na mazingira ya karne ya 21 na kuimarisha uwekezaji wa umma. Baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kusisitiza kuhusu utawala bora wakati wa ziara yake nchini Ghana, UNCTAD imesisitizia pia umuhimu wa utawala bora. Ripoti ya shirika hilo, inaonya kuhusu kuanzishwa kwa taasisi za maendeleo ya uchumi katika nchi masikini.
Gore, anasema Tanzania na Uganda zimeanzisha taasisi za sera ya uongozi na misaada, ambapo wananchi wanajionea wenyewe mafanikio ya misaada inayotolewa. Mwanauchumi huyo wa UNCTAD, anafafanua kuwa mipangalio ya ndani ya nchi inaleta maendeleo katika kuhakikisha kuwa misaada inatumika ipasavyo kwa maendeleo ya nchi yaliyokusudiwa. Rwanda kwa upande wake inatafuta njia ya kuanzisha mwonekano wa taifa hilo kwa kuwa na mikakati yake. Zambia inaainisha vipaumbele vya sekta zake katika mikakati ya kiushindani. Malawi imepata mafanikio kupitia mpango wake wa kutoa ruzuku ya mbolea ambayo imeiwezesha nchi hiyo kuwa na akiba nzuri ya chakula na hata kusafirisha chakula.
Baada ya kuwa na wastani wa asilimia 7 ya kukua kwa uchumi kwa mwaka kati ya 2002 na 2008, nchi zinazoendelea zimeathirika vibaya na msukosuko wa kiuchumi. Na hiyo imetokana na kushuka bei kwa bidhaa, upunguzaji wa mahitaji kwa ajili ya bidhaa za kusafirisha nje na kushuka kwa mapato ya utalii.
UNCTAD inaamini kuwa uchumi wa nchi masikini unaweza kupanda tena, kwa kutekeleza maendeleo mapya ya nchi husika kulingana na mazingira ya karne ya 21.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (IPS)
Mhariri: Othman Miraji