1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNESCO yaapa kuisaidia Mali kulinda Turathi ya Dunia

Admin.WagnerD4 Julai 2012

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (UNESCO) pamoja na ujumbe wa serikali ya Mali umelaani uharibifu unaofanywa na waasi nchini Mali; na uko mbioni kutuma wawakilishi wake ili kutathmini Timbuktu.

https://p.dw.com/p/15R7V
Msikiti huu uliopo Mali ulijengwa kati ya karne ya 15 na 16.
Msikiti huu uliopo Mali ulijengwa kati ya karne ya 15 na 16.Picha: Getty Images

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (UNESCO) na wawakilishi wa serikali ya Mali wamelaani uharifu wa maeneo ya turathi ya Dunia uliofanyika katika mji wa Timbuktu. Na pande hizo mbili zimeahidi kutuma ujumbe mjini humo ili kutathmini kiwango na madhara ya uharibifu huo.

Akizungumza mjini St. Petersburg, Urusi Waziri wa Utamaduni wa Mali Fadima Toure Diallo, ameelezea uharibifu huo uliofanywa na waasi wa kiislamu katika maeneo hayo kama vitendo vya kikatili na kinyama.

Serikali ya Mali: Mashambulizi haya yanakiuka maadili yetu

Diallo amesema raia wa Mali ni watu wanaoheshimu dini, na serikali inaheshimu dini pia. Ameongeza kusema kwamba mashambulizi hayo yamelenga uadilifu wa Mali na utamaduni wake.

Piramidi hili ni moja ya vivutio mjini Timbuktu.
Piramidi hili ni moja ya vivutio mjini Timbuktu.Picha: DW

Mustakabali wa mahekalu ya mjini Timbuktu ilikuwa ajenda mojawapo ya mkutano huo wa 36 wa Kamati ya Turathi wa Dunia, uliofanyika nchini Urusi na ambao unafikia tamati yake wiki hii.

Uharifu huo unaoendelea katika misikiti na makaburi makubwa nchini Mali, unaonesha kwa mara nyingine tena kuwa shirika hili la Unesco halina nguvu ya kukomesha kile kilichokiita kitendo cha uharibifu kilichokithiri.

Unesco ina msimamo gani?

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Unesco, Irina Bokova, amesema hali hii inafuatia jitihada za hali na mali za shirika hilo, kama anavyofafanua hapa.

"Tuna wasiwasi sana na yanayotokea nchini Mali. Tuna wasiwasi hasa na uharifu huo . Kwa upande mmoja ni eneo la turathi ya Dunia, makaburi yao makubwa, misikiti yao, kumbukumbu zao za maandishi ambazo bado hazijachapishwa na inayowasilisha thamani kubwa kwa utu, na yanayotokea huko hayakubaliki kabisa." Amesema Bokova.

Katika taarifa yake, Kamati ya Urithi wa Dunia imelaani uharibifu huo unaoendelea na kumtaka Mkurugenzi Mkuu Bokova kuunda mfuko maalum kwa ajili ya nchi ya Mali, ambao utaisaidia nchi hiyo kutunza minara yake ya pekee kabla ya uharibifu mkubwa zaidi kutokea.

Mji wa Timbuktu umesheheni utajiri wa historia ya kale.
Mji wa Timbuktu umesheheni utajiri wa historia ya kale.Picha: dpa

Historia ya Mto Bahiyah isije kujirudia Timbuktu

Unesco inaamini kuwa juhudi za haraka na za pamoja zinaweza kuzuia uharibifu mkubwa zaidi na hivyo kulinda turathi hiyo kwa manufaa ya kizazi kijacho. Kwa kufanya hivi, uharibifu kama ulioshuhudiwa katika Mto Bamiyah, Afghanistan ambao ulifanywa na wanamgambo wa Taliban miaka 11 iliyopita hautajirudia huko Afrika ya Magharibi.

Kitu ambacho Unesco inaweza kukifanya ni kuomba uharibifu huu ukomeshwe. Shirika hili linashajiisha uungaji mkono wa kimataifa kutoka kwa viongozi wa kisiasa na kidini ili janaga hili lote ambalo naamini ni janga kwa binaadamu wote , ulisitishwe, amesisitiza.

Timbuktu ni mji ulioorodheshwa kuwa eneo la Turathi ya Dunia tangu mwaka 1988. Waislam wenye msimamo mkali wameharibu makaburi makubwa 16 mjini humo mwishoni mwa wiki. Aidha, mji huo una maktaba nyingi zinazohifadhi maandishi na nyaraka muhimu za dini ya kiislamu.

Mwandishi: Pendo Paul

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman