1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaItaly

UNHCR yasema wahamiaji 186,000 wameingia Ulaya mwaka 2023

29 Septemba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR limesema takriban watu 186,000 wameingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4Wx20
Lampedusa, Italia
Maelfu ya wahamiaji hutumia njia hatari kuvuka bahari kujaribu kuingia Ulaya. Picha: YARA NARDI/REUTERS

Mkurugenzi wa ofisi ya UNHCR mjini New York Ruven Menikdiwela, ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba wahamiaji 130,000 wameandikishwa nchini Italia, idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 83 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Menikdiwela ameeleza kuwa, zaidi ya watu 2,500 hawajulikani waliko au wamekufa tangu kuanza kwa mwaka huu. Hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, IOM lilitoa takwimu zilizoonyesha kuwa zaidi ya watu 2,700 hawajulikani waliko au wamekufa wakijaribu kuingia Ulaya.

Ongezeko la idadi ya wahamiaji tayari limesababisha mivutano ndani ya Umoja wa Ulaya juu ya sera na hatua zinazofaa kuchukuliwa ili kudhibiti wimbi la wahamiaji.

Mataifa ya Ulaya yamekuwa yakizozana kuhusu suala la kugawana wakimbizi. Viongozi wa nchi za Ulaya wanakutana leo nchini Malta kujadili suala la wahamiaji.