UNITED NATIONS:Ban Ki Moon kukutana na AU
15 Aprili 2007Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon anafanya mazungumzo hapo kesho ya ngazi za juu na wawakilishi wa Umoja wa Afrika ili kujadilia suala la Darfur.Lengo la mkutano huo ni kutafuta mbinu ya kupeleka majeshi ya kulinda amani katika eneo linalokumbwa na vita la Darfur nchini Sudan.
Katibu Mkuu huyo anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Alpha Oumar Konare ili kujaribu kufikia makubaliano ya kupeleka kikosi cha majeshi alfu 2300 ya Umoja wa Mataifa ili kushirikiana na majeshi ya Umoja wa Afrika yaliyoko Darfur .Hatua hiyo iliidhinishwa kimsingi ila utekelezaji bado unasuasua japo majeshi ya Umoja wa Afrika yanakumbwa na uhaba mkubwa wa fedha na vifaa.
Matokeo ya mazungumzo hayo yanatarajiwa kutangazwa kesho mchana kulingana na msemaji wa Katibu Mkuu Bi Marie Okabe.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katia eneo la Darfur Jan Eliasson na mwenzake Dr Salim Ahmed Salim wanatarjiwa kuelezea Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa hatua zilizofikiwa baada ya makubaliano kufikiwa mwezi Mei kati ya serikali ya Sudan na waasi wa Darfur.
Mikutanoi hiyo inapangwa kufanyika wakati juhudi za kidiplomasia za kujaribu kumaliza mgogoro wa Darfur zikishika kasi.Vita katika eneo hilo vimesababisha vifo vya takriban watu laki mbili na kuacha wengi wapato milioni 2 bila makao kulingana na takwimu za Umoja wa mataifa.
Wakati huohuo afisa mmoja wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika AU amepigwa risasi hadi kufa katika eneo la El Fasher lililoko Darfur.Kwa mujibu wa msemaji wa ujumbe huo,hicho ni kifo cha saba cha wanajeshi hao kutokea mwezi huu.