UN:Wapiganaji wa IS bado wanaendelea na operesheni zao
25 Agosti 2020Mkuu wa kukabiliana na ugaidi wa Umoja wa Mataifa, Vladimir Voronkov amesema zaidi ya wapiganaji 10,000 wa kundi la itakadi kali linalojiita Dola la Kiislamu, IS, bado wanaendeleza operesheni zao nchini Iraq na Syria.
Voronkov ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa wapiganaji wa IS wanafanya shughuli zao kwa uhuru ndani ya nchi hizo mbili, miaka miwili tangu kundi hilo lilipoteza udhibiti kamili wa maeneo iliyokuwa ikiyashikilia.
''Toka mwanzoni mwa mwaka huu, tumeshuhudia mchanganyiko wa vitisho kwenye kanda hiyo. Kwenye maeneo ya mizozo vitisho viliongezeka, mfano wa makundi ya IS ambayo yalizidisha shughuli zake nchini Irak na Syria na kwenye maeneo mengine ya kikanda. Na kwenye maeneo ambako hakuna mizozo, kitisho kimepungua kwa muda mfupi''.
Shughuli za IS wakati wa Covid-19
Voronkov anaelezea kwamba janga la Covid-19, lilichangia katika kupunguza mashambulizi ya kigaidi kwenye nchini nyingi, kutokana hasa na vizuwizi vilivyowekwa na serikali katika kupambana na janga hilo.
Mkuu huyo wa kupambana na ugaidi wa Umoja wa Mataifa, amesema kwamba janga la Covid-19 limeangazia changamoto za kupambana na kitisho cha ugaidi. Akielezea shughuli za kundi la IS na makundi mengine ya kigaidi yanayojaribu kutumia matokeo mabaya ya kiuchumi na kisisasa yaliosababishwa na janga la Covid-19 katika kuendesha propaganda zao.
Propaganda za IS barani Afrika
Kwa mujibu wa afisa huyo wa Umoja wa Mataifa, makundi ya itikadi kali yamekusanyika upya na sasa yanaendesha operesheni hadi nje ya mipaka ya mataifa yaliyo kwenye machafuko ya Iraq na Syria. Voronkov ameonya kuwa propaganda za kundi la IS zinaendelea kupata wafuasi kwenye maeneo mengi duniani huku ikiwemo barani Afrika hususani kwenye mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso.
Kuhusu Afrika Magharibi, Voronkov amesema kwamba kundi hilo la IS lina wapiganaji 3 500, likiwa moja wapo ya majimbo muhimu yalio mbali ya kundi hilo. Hivi sasa kundi hilo la kigaidi la IS, lina wapiganaji wachache nchini Libya.
Huku likitumia tofauti za kikabila kundi hilo la IS ni tishio kubwa la kikanda huko barani Afrika. Voronkov alielezea pia wasiwasi wake kuhusu mashambulizi yanayoendeshwa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Msumbiji.
Voronkov amesema barani Ulaya, itikadi kali zinatumiwa kupitia mitandao, akiyataja mashambulizi matatu ya IS yaliochochewa kupitia mitandao, moja nchini Ufaransa na mawili nchini Uingereza.