Upinzani Afrika waipongeza Mahakama ya Juu ya Kenya
4 Septemba 2017Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai aliwaeleza maelfu ya wafuasi wake katika mkutano wa hadhara mwishoni mwa wiki kuwa iwapo hilo limefanyika Kenya basi linaweza kufanyika Zimbabwe pia.
Tsvangirai ambaye ni kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) amejaribu mara tatu kuwania nafasi ya urais kupitia chaguzi zilizofanyika nchini Zimbabwe lakini amekuwa akishindwa katika chaguzi hizo na Rais Robert Mugabe ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1980.
Chaguzi nchini Zimbabwe mara nyingi zimekuwa zikigubikwa na vurugu, vitisho na mashitaka ya ukiukwaji wa tararibu za uchaguzi. Tshangirai amesema huu ni mfano wa kuigwa barani Afrika na kuwa ni hatua moja nzuri katika kufikia demokrasia ya kweli barani Afrika.
Ijumaa iliyopita mahakama ya juu ya Kenya ilifuta matokeo ya uchaguzi wa rais wa Novemba 8 yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kufuatia mahakama hiyo kuthibitisha kasoro nyingi katika zoezi la uchaguzi huo na kuagiza uchaguzi ufanyike baada ya siku 60 ambapo sasa uchaguzi huo unatararajiwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu.
" Majaji wa Kenya wametoa fundisho barani Afrika na duniani kwa ujumla" alisema kiongozi wa upinzani nchini Burundi Charles Nditije.
Burundi inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa tangu April 2015 wakati Rais Pierre Nkurunziza alipotangaza nia yake ya kuwania muhula wa tatu wa uongozi ambapo alishinda uchaguzi uliofanyika mwezi Julai uliosusiwa na upinzani wakidai kuwa ni ukiukaji wa katiba.
Nditije anayeoongoza muungano wa vyama vya upinzani - CNARED alisema kilichofanyika Kenya ni tofauti na yaliyotokea nchini Burundi na kusisitiza kuwa uamuzi wa mahakama ya juu ya Kenya ni mfano mzuri wa uhuru wa mahakama unaotakiwa kuigwa.
Upinzani Uganda nao wasifia mahakama ya juu ya Kenya
Uganda ambayo iko chini ya utawala wa Rais Yoweri Kaguta Museveni tangu mwaka 1986 kiongozi wa chama cha upinzani nchini humo Kizza Besigye alipongeza uamuzi wa mahakama ya juu ya Kenya akisema ni mfano wa kuigwa barani Afrika . Besigye alitiwa mabaroni, wakati na baada ya uchaguzi wa Februari mwaka 2016 ambapo alishika nafasi ya pili katika uchaguzi uliogubikwa na utata.
Museveni anayeliongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kwa miaka 31 alishinda duru ya kwanza ya uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 60 ya kura zilizopigwa lakini hata hivyo waangalizi wa uchaguzi kutoka nje walisema uchaguzi huo ulifanyika katika mazingira ya vitisho na kuongeza kuwa ushindi wa Museven ulitokana na udanganyifu na vitisho.
Nchini Tanzania mbunge wa upinzani nchini humo Zito Kabwe alitoa mwito wa kufanyika kwa marekebisho ya katiba nchini humo akisema Kenya imepiga hatua kubwa na kuwa Tanzania inahitaji katiba mpya ili kuwepo na uwezekano wa kupinga matokeo ya uchaguzi kupitia mahakama.
Nchini Rwanda ambako Rais Paul Kagame alichaguliwa tena kushika muhula wa tatu kwa asilimia 99 ya kura mwezi uliopita,Kiongozi wa upinzani Frank Habineza alisema uamuzi wa mahakama ya juu ya Kenya unatia moyo kwa upinzani barani Afrika. Alisema uhuru wa mfumo wa mahakama ni munhimu barani Afrika na unasaidia kuzuia hatua nyingine mbadala za kupinga matokeo hayo kama vile kuanzisha makundi ya upinzani yenye silaha ili kudai haki.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE
Mhariri Mohammed Abdul-Rahman