1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Misri waitisha maandamano zaidi

10 Desemba 2012

Mzozo wa kisiasa nchini Misri unaonekana kuzidi kupanuka, baada ya kikundi muhimu cha upinzani kuitisha maandamano makubwa kupinga kura ya maoni juu ya mswada wa katiba, ambayo inatarajiwa kupigwa tarehe 15 Desemba.

https://p.dw.com/p/16yyS
National Salvation Front
National Salvation FrontPicha: AFP/Getty Images

Hayo yanajiri licha ya hatua ya Rais Mohammed Mursi kuondoa sheria aliyokuwa amepitisha kujilimbikizia madaraka. Katika tangazo lililotolewa kwa vyombo vya habari na kikundi kikubwa cha upinzani nchini Misri, National Salvation Front, kikundi hicho kimesema kinaipinga kura ya maoni juu ya mswada wa katiba, kwa sababu kinaamini kwamba itasababisha mgawanyiko na migogoro zaidi.

Kikundi hicho kimeitisha maandamano makubwa kesho Jumanne katika miji yote ya nchi hiyo, kuupinga mswada huo ambao kwa kiwango kikubwa uliandikwa na tume inayodhibitiwa na wanasiasa wa kiislamu.

Mohamed ElBaradei, kiongozi wa kikundi kilichoitisha maandamano mapya
Mohamed ElBaradei, kiongozi wa kikundi kilichoitisha maandamano mapyaPicha: dapd

Uamuzi wa pupa

''Kuitisha kura ya maoni wakati nchi ikikumbwa na mivutano, kunadhihirisha jinsi serikali inavyofanya mambo kwa pupa'', kilidai kikundi hicho cha upinzani. Kikundi hicho kinaongozwa na mwanasiasa maarufu Mohammed el-Baradei, ambaye kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, amesema, ''Tutaiangusha katiba ambayo haitilii maanani haki zetu na uhuru wetu''.

Upinzani unasisitiza kwamba katiba hiyo inapuuza haki za msingi na uhuru wa wanawake. Ikiwa wananchi wa Misri wataikataa katiba hiyo katika kura ya maoni ya tarehe 15 Desemba, Rais Mohammed Mursi ataitisha uchaguzi katika kipindi cha miezi mitatu, kuchagua baraza jipya la wawakilishi.

Maandamano mkabala

Kikundi cha Udugu wa Kiislamu ambacho ndicho anachotoka rais Mursi kimeunga mkono uamuzi wake, na kuwataka wapinzani kuepuka kile kilichokiita matatizo yasio na msingi. Msemaji wa kikundi hicho Mahmoud Ghuzlan amesema raia wote wa Misri wanapaswa kuupigia kura mswada wa katiba, na kuongeza kuwa kura hiyo inapaswa kupigwa kwa tarehe iliyopangwa, bila mabadiliko wala kucheleweshwa.

Misri imekumbwa na maandamano makubwa mnamo wiki mbili zilizopita
Misri imekumbwa na maandamano makubwa mnamo wiki mbili zilizopitaPicha: Reuters
Rais wa Misri Mohammed Mursi
Rais wa Misri Mohammed MursiPicha: AP

Watu saba walipoteza maisha yao Jumatano wiki iliyopita, katika maandamano mengine yaliyowakutanisha watu wanaounga mkono kambi tofauti za kisiasa.

Muungano wa vyama vya kiislamu umesema utafanya maandamano makubwa kesho Jumanne kumuunga mkono rais Mursi, hii ikiwa ni kwa mujibu wa tovuti ya gazeti linalomilikiwa na serikali.

Hakuna dalili ya suluhu

Watu kutoka kambi zinazokinzana kisiasa walipiga kambi nje ya Ikulu ya rais mjini Cairo kwa siku tatu mfululizo, na waandamanaji zaidi walijiunga nao Jumapili. Wiki iliyopita, eneo hilo lilishuhudia makabiliano yenye ghasia baina ya waandamanaji wanaompinga rais na wale wanaomuunga mkono.

Misri imekumbwa na maandamano makali mnamo wiki mbili zilizopita, kumshinikiza rais Mohammed kubatilisha uamuzi alioutangaza tarehe 22 Novemba, kupanua madaraka yake na kuahirisha kura kuhusu katiba. Huo ndio mzozo mkubwa zaidi kuikumba nchi hiyo tangu kuchaguliwa kwa rais Mursi mwezi June mwaka huu. Ingawa Mursi aliiondoa shereia hiyo mwishoni mwa juma, waandamanaji wa upinzani tayari wameanza kumtaka aondoke kabisa madarakani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/DPA
Mhariri: Hamidou Oummilkheir