1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani, muungano tawala wote wadai ushindi uchaguzi DRC

31 Desemba 2018

Upinzani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo umesema unatarajia moja ya wagombea wao atashinda uchaguzi wa rais kwa kuzingatia matokeo ya awali, lakini muungano tawala umesema una imani mgombea wake ameshinda uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/3AoTb
Kongo hält mit zwei Jahren Verspätung historische Wahlen ab
Picha: Reuters/K. Katombe

Madai hayo kinzani yanafuatia uchaguzi wenye vurugu siku ya Jumapili ambamo Wacongo wengi walishindwa kupiga kura kutokana na mripuko wa Ebola, migogoro na matatizo ya usafirishaji.

Kura hiyo ilinuwiwa kumchagua mrithi wa rais anaeondoka Joseph Kabila, baada ya miaka 18 madarakani na huenda ikaipeleka nchi hiyo ya Afrika ya Kati katika mabadiliko ya kwanza kabisaa ya kisiasa kwa njia ya kidemokrasia.

Matokeo yoyote yanayobishaniwa yanaweza kusababisha marudio ya vurugu zilizofuatia uchaguzi wa mwaka 2006 na 2011, na kuporomoka pakubwa kwa hali ya usalama, hasa kwenye maeneo ya mpakani mwa Congo na Rwanda, Uganda na Burundi, ambako makundi kadhaa ya wapiganaji yako mashughuli.

Kongo hält mit zwei Jahren Verspätung historische Wahlen ab
Felix Tshisekedi,kiongozi wa chama cha upinzani cha UDPS akipiga kura yake mjini Kinshasa.Picha: Reuters/O. Acland

Kila upande wadai ushindi

Vital Kamerhe, meneja kampeni wa mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi, alisema mapema kwamba hesabu za mwanzo zinamuonyehsa Tshisekedi na mgombe mwingine mkuu wa upinzani Martin Fayulu wakikabana koo katika uongozi, wote wakiwa na asilimia 40 ya kura.

Alisema mgombea wa muungano unaotawala, Emmanuel Ramazani Shadary, anaeungwa mkono na Rais Kabila, alikuwa na asilimia 13 tu, ingawa sehemu kubwa ya kura bado haijahesabiwa. Uchaguzi huu ndiyo wa kwanza usiyo na duru ya marudio.

Nehemia Mwilanya, mkuu wa shughuli za ikulu wa rais Kabila na mjumbe wa kampeni ya Shadary, aliuambia mkutano wa habari Jumatatu asubuhi kwamba alikuwa na uhakika Shadry ameshinda, ingawa hakutoa takwimu makhsusi. "Kwetu, ushindi ni wa uhakika," alisema Mwilanya.

Fayulu: Kambi ya Shadary inaota

Kambi ya Fayulu bado haijatoa takwimu makhsusi lakini Fayulu alisema Jumapili jioni kwamba kambi ya Shadary ilikuwa 'inaota' ikiwa inadhani itashinda. Uchunguzi wa karibuni zaidi wa maoni ya wapigakura, uliotangazwa na taasisi ya utafiti wa Congo ya chuo kikuu cha New York siku ya Ijumaa, ulionyesha kuwa Fayulu, meneja wa zamani wa kampuni ya Exxon Mobil, alikuwa akiongoza kwa asilimia 47.

Kongo Beni improvisierte Wahl
Wakaazi wa Beni wakishiriki kura ya dhihaka kupinga hatua ya CENI kufuta uchaguzi katika eneo hilo.Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Kudra Maliro

Tshisekedi alikuwa na asilimia 24 na Shadary asilimia 19. Matokeo ya kwanza ya awali yanatarajiwa kutolewa na tume ya uchaguzi (CENI) siku ya Jumanne.

Siku ya uchaguzi ilikuwa tulivu kwa sehemu kubwa licha ya matukio kadhaa ya vurugu, ikiwemo ugonvi katika kituo cha kupigia kura mashariki mwa Congo ambamo watu wasiopungua watatu waliuawa.

Beni wapiga kura ya dhihaka

Zaidi ya Wacongo milioni 1.2 pia hawakuweza kutumia haki yao ya kupiga kura katika maeneo matatu ya ngome za upinzani, ambako CENI ilifuta uchaguzi wiki iliyopita, ikitoa sababu za mripuko unaoendelea wa ugonjwa wa Ebola na vurugu za kikabila.

Hata hivyo, katika eneo lenye mripuko mkubwa wa Ebola la Beni, ambalo pia ni ngome ya upinzani, wakaazi waliendesha uchaguzi wa rais wa dhihaki kuzionyesha mamlaka kwamba uamuzi wa kuahirisha kura katika eneo hilo kutokana na mripuko wa Ebola haukuwa na msingi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Sekione Kitojo