Mgombea wa chama cha NUP, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, mgombea wa FDC Patrick Oboi Amuriat na jenerali Mugisha Muntu wa ANT wamesisitiza kwamba uchaguzi huu ni muhimu sana kwa Uganda na watafanya kila juhudi kulinda kura zao kwa pamoja.
Hii ni kwa sababu wana imani kwamba rais Museveni mara hii hawezi kupata asli mia 50 na kura moja ili kutangazwa mshindi wa duru ya kwanza.
Wagombea hao wamelezea kuwa ikiwa mmoja wao atapata kura nyingi na kulazimisha duru ya pili ya uchaguzi, wengine wote watamuunga mkono.
Imani ni kubwa ya kunyakua ushindi
Wagombea hao wameelezea kuwa licha ya madhila waliotendewa na utawala katika kipindi cha kampeni wameweza kuwahamasisha wapiga kura kufahamu kuwa uchaguzi huu utakuwa wenye mapinduzi makubwa ikiwa watajitokeza kwa wingi kuwapigia kura.
Hii ni kwa msingi kwamba hapo awali chama cha NRM kimeweza kushinda watu wakiwa hawana imani kuwa uchaguzi huo una maana yoyote kutokana na upinzani kutoungana.
Aliyekuwa mgombea urais katika chaguzi zilizopita Dkt Kiza Besigye amewahimiza wapiga kura kuzingatia kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19.
Ametoa angalizo kuwa ijakuwa kanuni hizo zimetumiwa kukandamiza upinzani kisiwe kisingizio cha kuwazuia watu kufuatilia zoezi la kuhesabiwa kwa kura.
Leo Jumanne ndiyo siku ya mwisho ya kampeni na tume ya uchaguzi imelegeza kanuni za kuzuia watu kwenda na simu au kupiga picha kwenye vituo vya uchaguzi.