Upinzani wa Kenya wataka Umoja wa Afrika upeleke majeshi ya kulinda amani
3 Februari 2008Upinzani nchini Kenya umeutaka Umoja wa Afrika upeleke wanajeshi wa kulinda amani kumaliza machafuko yanayoendelea nchini humo.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amesema umwagaji damu unaoendelea unatisha huku polisi wakiripoti vifo vya watu 47.
Odinga amesema chama chake kimejitolea kwa dhati kushiriki kwa mazunguzo ya kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo unaoendelea nchini Kenya na kutaka mateso dhidi ya raia yakome.
Aidha kiongozi huyo amesema chama chake cha Orange Democratic movement, ODM, hakitajondoa katika mazungumzo yanayoongozwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan. Mazungumzo hayo yataingia awamu muhimu hapo kesho.
Wakati huo huo, maelfu ya wakaazi wa magharibi mwa Kenya wamekimbia operesheniy a polisi, siki moja baada ya watu kadhaa kuuwawa kwenye machafujko mapya yanayotishia juhudi za kumaliza majuma ya machafuko nchini humo.
Wanaume, vijana na akina mama wamekimbilia maeneo ya milimani huku maafisa wa polisi wakisaka silaha zilizoibwa katika eneo la Ainamoi karibu na mjini Kericho.
Operesheni hiyo ya polisi inafanywa kufuatia mauaji ya afisa mmoja wa polisi wakati maelfu ya wakaazi walipoivamia ofisi ya serikali Ijumaa iliyopita na kuiba bunduki nne na mamia ya risasi.