1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wapania kugomea biashara zenye mafungamano na serikali ya Kibaki.

18 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CuOU

Upinzani nchini Kenya umesema utaanzisha mgomo wa kiuchumi dhidi ya kampuni zilizo na mafungamano na serikali baada ya kuongoza maandamano ya mwisho hii leo kuhusu matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 27 mwezi uliopita.

Msemaji wa serikali ya Kenya dakta Alfred Mutua amepuuza njama hiyo ya upinzani akisema kila mkenya ana haki ya kufanya atakavyo lakini mkakati huo hautafaulu.

Polisi wa kupambana na fujo na wanajeshi wa vikosi maalumu wameshika doria mjini Nairobi na katika ngome za upinzani magharibi mwa Kenya.

Duru za polisi zinasema watu wasiopungua 14 wameuwawa katika maandamano ya siku tatu yaliyoiotishwa na upinzani.

Leo wapatanishi wawili wamefanya mazungumzo na viongozi wa upinzani kujaribu kuutanzua mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini Kenya.

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, amekutana na Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, na rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, na kuwaeleza matakwa ya chama chake cha ODM kwa rais Kibaki.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, anatarajiwa kuwasili mjini Nairobi Jumanne wiki ijayo.