1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, Afrika Kusini zatetea mazoezi ya kijeshi na China

23 Januari 2023

Afrika Kusini na Urusi zimetetea uamuzi wa kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na China mwezi Februari, huku Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, akianza ziara yake nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/4MarT
Südafrika Besuch Außenminister Lawrow Russland
Picha: Russian Foreign Ministry Press Service via AP

Lavrov aliwasili siku ya Jumatatu (Januari 23) kwenye mji mkuu wa Afrika Kusini, ambako alipokewa na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Afrika Kusini, Naledi Pandor.

Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, waziri huyo wa mambo ya nje wa Urusi alisema suala la mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya washirika hao watatu halina utata na asingelipenda kamwe lihusishwe na kashfa yoyote.

Lavrov aliongeza kwamba nchi yake imeshatoa "taarifa zote muhimu juu ya mipango yake kwenye mazoezi hayo ya kijeshi", ambayo yamekosolewa vikali na mataifa ya Magharibi na washirika wao. 

Soma zaidi: Lavrov: Nchi za Magharibi zilizuia mazungumzo ya kumaliza vita Ukraine

Baadhi ya vyama vya upinzani nchini Afrika Kusini na jamii ndogo ya raia wa Ukraine wanaoishi nchini humo wanaipinga ziara ya Lavrov katika taifa hilo linalosema haliegemei upande wowote kwenye mgogoro baina ya Urusi na Ukraine na hata kuwahi kuomba kuwa mpatanishi wake.

Afrika Kusini yashikilia msimamo wake

Waziri Pandor aliwaambia waandishi wa habari kwamba nchi yake inaendelea kushikilia msimamo wake wa kuwa tayari kuunga mkono suluhisho la amani kwa migogoro ya ndani ya Afrika na ya kwengineko ulimwenguni. 

Südafrika Besuch Außenminister Lawrow Russland
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Naledi Pandor (kulia) akiwa na mgeni wake, Waziri wa Mmabo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Pretoria siku ya Jumatatu (Februari 23).Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Hata hivyo, Lavrov alidai kuwa nchi yake daima imekuwa tayari kwa majadiliano, lakini ni upande wa  Ukraine ndio unaokataa mazungumzo ya amani, jambo aliloonya kwamba linafanya iwe vigumu zaidi kuutatuwa mzozo wenyewe.

Ukraine na Marekani zinadai hazioni ishara yoyote ya Moscow kutaka kweli mazungumzo, badala yake zinaishuku kuwa inatumia mbinu hiyo kujipanga upya baada ya kile zinachosema ni kushindwa vibaya kwenye uwanja wa vita.

Soma zaidi: Urusi yafanya mashambulizi kutaka kuukamata mji wa Bakhmut

Licha ya kwamba Afrika Kusini ina kiwango kidogo cha biashara na Urusi, lakini inazingatiwa kuwa kinara wa mtazamo unaoungwa mkono na China na Urusi ambao unataka dunia yenye mihimili mingi ya nguvu badala ya ulimwengu wa sasa unaotawaliwa na nguvu moja tu ya Magharibi, hasa hasa Marekani. 

Pandor alisisitiza kwenye mkutano huo na waandishi wa habari kwamba nchi yake haitaburuzwa iegemee upande wowote, na badala yake ameyakosoa mataifa ya Magharibi kwa kuilaani kwake Urusi huku yakipuuzia masuala mengine kama vile ukaliaji wa mabavu wa Israel kwenye ardhi ya Wapalestina.

Soma zaidi: Lavrov: Magharibi na Ukraine zataka kuiangamiza Urusi

Jeshi la Afrika Kusini linapanga kuanza mazoezi yake ya pamoja na China na Urusi katika pwani ya mashariki mnamo tarehe 17 hadi 27 Februari, hatua inayotazamiwa kuyatikisa zaidi kati ya taifa hilo kubwa kiuchumi barani Afrika na Marekani na nchi za Ulaya. 

Vyanzo: Reuters, AFP