Urusi, Belarus zasaini makubaliano juu ya silaha za nyuklia
25 Mei 2023Hatua hiyo iliyofikiwa Alhamisi inafuatia mapatano ya awali yaliyoafikiwa baina ya Rais Vladimir Putin na mwenzake wa Belarus, Alexander Lukashenko.
Putin mnamo mwezi Machi alitangaza kwamba nchi yake inapanga kupeleka silaha za nyuklia za kimkakati na masafa mafupi nchini Belarus. Kutiwa saini makubaliano hayo kunafanyika wakati ambapo Urusi inajiandaa kwa mashambulizi ya kulipa kisasi ya Ukraine.
Maafisa wa Urusi na Belarus wanasema hatua hiyo imetokana na chuki za nchi za Magharibi.
Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kuhusiana na lini silaha hizo zitakapopelekwa ila Rais Putin alisema kuwa ujenzi wa maghala ya silaha hizo huko Belarus utaanza Julai mosi. Kiongozi wa upinzani wa Belarus aliye uhamishoni, Svetlana Tsikhanouskaya, amelaani hatua hiyo.
Haya yanajiri wakati Ukraine ikitarajiwa kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Urusi, katika juhudi za kuyakomboa maeneo ya mashariki ya Ukraine yanayokaliwa na Urusi.