1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, Iran, Uturuki zawania kupata msimamo wa pamoja Syria

Sekione Kitojo
3 Aprili 2018

Mataifa makubwa matatu yanayohusika na sura ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria, Iran, Urusi na Uturuki yajadili njia za  kumaliza mapigano nchini humo licha ya uhusika wao katika kampeni za kijeshi ndani ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/2vQTW
Türkei Recep Erdogan & Wladimir Putin in Ankara | Grundsteinlegung-Zeremonie Akkuyu AKW
Picha: Reuters/U. Bektas

Viongozi  wa  mataifa  hayo  matatu Vladimir Putin, Recep Tayyip Erdogan  na Hassan Rouhani  wa  Iran watakutana  mjini  Ankara kwa  mazungumzo  yatakayohusu  katiba  mpya  ya  Syria  na kuongeza  usalama  katika maeneo ambayo  yametengwa  bila  ya shughuli  za  kijeshi  nchini  humo, wamesema  maafisa  wa  Uturuki.

Türkei Recep Erdogan & Wladimir Putin in Ankara
Rais Erdogan(kushoto) na mgeni wake rais Putin wa Urusi mjini AnkaraPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Ozbilici

Mkutano  huo  wa  kilele  kuhusu  Syria  unawaleta  pamoja  mataifa mawili  yenye  nguvu  ambayo  yamekuwa  waungaji  mkono wakubwa  wa  rais Bashar al-Assad , Iran  na  Urusi , pamoja  na mmoja  kati  ya  wapinzani  wake  wakubwa  Uturuki.

Ushirikiano  baina  ya  kambi  hizo  zinazopingana unaongeza matumaini  ya  kuiimarisha  Syria  baada  ya  miaka  saba  ya  mzozo ambamo  watu 500,000 wameuwawa  na  nusu  ya  wakaazi wamekimbia  makaazi  yao.

Lakini  ghasia  zimeendelea, zikiakisi  misimamo  tofauti  baina ya mataifa  hayo  matatu, ambayo bila  ya  kuwepo  kwa  uingiliaji  kati wa  mataifa  ya  magharibi, wanashikilia  mustakabali  wa  Syria kwa kiasi  kikubwa  katika  mikono  yao.

Jeshi  la  Syria  na  wanamgambo  wanaoungwa  mkono  na  Iran , wakiwa  na  msaada  wa  ndege  za  kivita  za  Urusi, wamekandamiza  wapinzani  karibu  na  mji  mkuu Damascus  katika eneo  la  Ghouta Mashariki moja  kati  ya  maeneo manne yanayoelezewa  kama  ni  kanda  zitakazokuwa   hazina shughuli  za kijeshi.

Türkei Recep Erdogan & Wladimir Putin in Ankara
Rais Putin akipokewa na mwenyeji wake rais Edrogan (kushoto)Picha: Reuters/U. Bektas

Uturuki yashutumu  na  kufanya  mashambulizi

Uturuki , ambayo  ilishutumu  vikali  mashambulizi  dhidi  ya  Ghouta mashariki , ilifanya  operesheni  nayo  ya  kijeshi kuwaondoa wapiganaji  wa  Kikurdi  wa  YPG kutoka  katika  jimbo  la  kaskazini magharibi  la  Afrin. Uturuki  imeahidi  kuukamata  mji  wa  Tel Rifaat na  kuendelea  zaidi  upande  wa  mashariki, na  kuikasirisha  Iran.

"Pamoja  na  nia  iliyopo, hatua  za  Uturuki  nchini  Syria , iwapo  ni Afrin, Tel Rifaat  na  maeneo  mengine  ya  Syria, yanapaswa kusitishwa  haraka  iwezekanavyo," afisa  mwandamizi  wa  Iran amesema.

Iran imekuwa mshirika  ambaye  ametoa  usaidizi  mkubwa  kwa  rais Assad wakati  wote  wa  mzozo  huo. Wanamgambo  wanaoungwa mkono  na  Iran  kwanza  walilisaidia  jeshi  lake  kuwazuwia  waasi kusonga  mbele, wakifuatiwa  na  kuingia  kwa  Urusi  katika  vita hivyo  mwaka  2015, na  kubadilisha  wimbi  kuelekea  upande  wa Assad.

Syrien Ost-Ghouta
Rais Assad akifanya ziara Ghouta mashariki nchini SyriaPicha: picture-alliance/dpa/SalamPix

Rais Vladimir Putin  amewasili  leo mjini  Ankara kushiriki  katika sherehe  za  kuanza  ujenzi wa  kinu  cha  kwanza  cha  kinyuklia kitakachotumika kutoa nishati  na  mkutano  kuhusu  Syria kesho Jumatano.  Hii  ni  ziara  ya  kwanza  ya  Putin  nje  ya  nchi  tangu kuchaguliwa  tena mwezi  uliopita. Alikutana  na  rais Recep Tayyip Erdogan  wa  Uturuki  mara  nane  mwaka  2017 wakati  uhusiano baina  ya  nchi  hizo  mbili  ulipoanza kuimarika   kukiwa  na ushirikiano wa  masuala  ya  nishati  na  pia  ndani  ya  Syria, na wakati  Uturuki  ikikabili  hali  ngumu  katika  uhusiano  wake  na mataifa  ya  magharibi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman