Urusi: Mamia ya askari wa Ukraine wamejisalimisha
18 Mei 2022Wizara ya ulinzi ya Urusi imedai kwamba ndani ya saa 24 zilizopita, wapiganaji 694 wa Ukraine walijisalimisha, wakiwemo 29 waliojeruhiwa na kwamba idadi jumla ya askari hao imefikia 959 tangu Mei 16. Aidha taarifa hiyo imeongeza kwamba askari wanaohitaji msaada wa matibabu wamepelekwa hospitali katika mji wa Novoazovsk kwenye eneo linalodhibitiwa na Urusi.
Kyiv ina matumaini ya kubadilishana askari wake waliojisalimisha, lakini Urusi imedai kwamba haijathibitisha ikiwa watakuwa sehemu ya zoezi la kubadilishana wafungwa. Bunge la Urusi linapanga kuwasilisha azimio la kuzuia zoezi la kuwabadilisha wapiganaji, ambao walikuwa wamejificha kwa miezi kadhaa ndani ya kiwanda cha chuma cha Azovstal wakati mji wa Mariupol ulipokuwa chini ya mzingiro.
Awali, naibu waziri wa ulinzi wa Ukraine Hanna Maliar alisema kwamba mazungumzo ya kubadilishana wapiganaji yanaendelea huku pia juhudi za kuwaondoa askari wengine waliosalia katika kiwanda hicho zikiendelea.
''Shukrani kwa ulinzi uliowekwa na askari wa Mariupol, adui alizuiwa kutuma tena vikosi vyake, takribani askari 20,000. Adui hakuweza kuwasambaza tena katika mikoa mingine, kwa hivyo haikufaulu kuchukua haraka Zaporizhzhia.''
Mwezi uliopita, Urusi ilidai kuudhibiti mji wa Mariupol baada ya wiki kadhaa za kuuzingira, lakini mamia ya askari wa Ukraine walikuwa wamejificha kwenye handaki chini ya ardhi katika eneo kubwa la viwanda la Azovstal lililozuiwa na vikosi vya Urusi. Pande hizo mbili pia zimedai kusitisha mazungumzo ya kumaliza vita hapo siku ya Jumanne kutokana na suala hilo la uwezekano wa kubadilishana wafungwa.
Mpatanishi mkuu wa Kyiv katika majadiliano hayo Mykhailo Podolyak amesema kwamba hakuna maendeleo yatakayopatikana ikiwa Urusi haitambui hali halisi ilivyo. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy na walikubaliana kwamba "ufumbuzi wa kidiplomasia baina ya Urusi na Ukraine" ndio mwafaka wa mzozo huo.
Hayo yakijiri Sweden na Finland zimewasilisha rasmi maombi ya kujiunga na jumuiya ya kujihami NATO, hatua ambayo inachochewa na wasiwasi wa usalama juu ya uvamizi wa Urusi.
Wakati huohuo Tume ya Ulaya inatarajiwa hii leo kutangaza mapendekezo ya kuachana na uagizaji wa gesi kutoka Urusi. Miongoni mwa mapendekezo tarajiwa ni pamoja na malengo ya uzalishaji wa nishati mbadala, kuongeza kasi ya vibali vya miradi ya nishati ya kijani kama vile mitambo ya upepo, kutanua miundombinu ya haidrojeni na kupanua uagizaji wa gesi kutoka nje.