1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na biashara ya silaha barani Afrika

P.Martin3 Februari 2009

Kampuni ya serikali ya Urusi inayouza silaha katika nchi za kigeni "Rosoboronexport" inatazamia kuongeza biashara yake ya silaha na zana za kijeshi barani Kiafrika katika kipindi cha miaka minne hadi mitano ijayo.

https://p.dw.com/p/Gm1l

Habari hiyo imetolewa,licha ya madai kuwa Urusi inauza silaha kwa makundi yanayofanya biashara ya magendo.Kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa Rosoboronexport, kampuni hiyo imefufua uhusiano wake na nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikinunua silaha kutoka Soviet Union ya zamani. Katika miaka ya hivi karibuni Urusi imeona maendeleo katika ushirikiano wake wa kijeshi na teknolojia barani Afrika. Licha ya mashindano makubwa katika masoko ya dunia, biashara ya silaha ya Urusi katika nchi za nje,imeendelea kuimarika tangu mwaka 2001 na biashara hiyo ikafikia kipeo chake mwaka jana.Hayo alisisitiza naibu mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Kirusi Viktor Komardin.

Lakini mtafiti wa masuala ya Urusi,China na Afrika wa jopo la wataalamu mjini Accra,Ghana linalounga mkono uchumi wa masoko huria anasema, ingawa baadhi kubwa ya silaha za Urusi huuzwa kwa washirika wa zamani wa Vita Baridi,makundi ya chini kwa chini barani Afrika vile vile hupatiwa silaha ndogo za aina mbali mbali na hivyo huendeleza migogoro katili ya kienyeji katika bara hilo.

Lakini sasa kumechomoza mtindo mpya,kwani China yaonekana kuchukua nafasi ya Urusi kama muuzaji wa silaha ndogo.Komardin amekiri kuwa Bara la Afrika likiendelea kuwa eneo la migogoro, sasa mapigano yamehamia maeneo yenye utajiri wa madini. Anakubali kuwa biashara ya silaha inachochea zaidi migogoro,lakini anasema haikusababisha mizozo hiyo. Wachambuzi wanasema,hata ikiwa Urusi au nchi nyingine yo yote ile itaacha kuziuzia silaha nchi za Kiafrika, hiyo haitomaanisha kuwa migogoro itamalizika papo hapo.

Kwa maoni yao,makundi yanayohusika katika migogoro isiyomalizika barani Afrika, yatapata wauzaji wengine wa silaha bila ya shida. Wanasema, migogoro hiyo ni matokeo ya mchanganyiko wa matatizo ya ndani katika jamii za Kiafrika kama vile tofauti za kikabila na dini: kinyanganyiro cha madaraka na uchumi dhaifu bila ya kusahau maslahi ya makampuni ya kigeni barani Afrika.Kuna mifano ya kutosha ya migogoro iliyozuka katikati ya maeneo yenye utajiri wa almasi na madini mengine, kuanzia sehemu za magharibi hadi katikati na kusini mwa Afrika.

Ni vigumu sana kujua kiwango cha biashara haramu ya silaha inayofanywa na Urusi,lakini kwa kuzingatia idadi ya migogoro inayotapakaa barani Afrika,biashara hiyo haramu huenda ikawa ni asilimia 20 ya biashara rasmi. Kati ya mwaka 2000 na 2007 Urusi iliuza silaha zenye thamani ya dola bilioni 1.1 katika nchi za Kiafrika. Urusi ni muuzaji mkuu wa pili wa silaha duniani baada ya Marekani.