1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, Uturuki na Iran zaijadili Syria

14 Februari 2019

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amemueleza mwenzake wa Urusi Vladimir Putin kwamba watahitaji msaada wa Urusi kufuatia uamuzi wa Marekani wa kuyaondoa majeshi yake nchini Syria.

https://p.dw.com/p/3DOTk
Russland Iran Türkei Erdogan Putin Rohani Sotschi
Picha: Reuters/S. Chirikov

Erdogan na Putin wamekutana hii leo mjini Sochi kuijadili Syria. Awali, Erdogan alikiri kuwepo kwa hali ya sintofahamu kufuatia uamuzi huo wa Marekani. 

Akizungumza akiwa mjini Sochi nchini Urusi, Erdogan amesema ni muhimu kwao kushirikiana katika kukabiliana na changamoto hiyo mpya. Amesema hayo katika hotuba yake iliyorushwa kwenye televisheni wakati wa mkutano wa kilele baina ya Urusi, Uturuki na Iran uliolenga kujadili mustakabali wa mzozo wa Syria. Rais wa Iran, Hassan Rouhani pia amehudhuria.

Uturuki imeiomba Urusi kushirikiana na vikosi vyake vilivyopo kwenye kambi ya jeshi la anga la Urusi ya Khmeimim iliyoko magharibi mwa Syria. Uturuki inataka kuweka ukanda salama karibu na mpaka wake ili kuondosha wasiwasi wa kiusalama.

Erdogan amesema hatua hiyo ya Marekani ya kuyaondosha majeshi yake Syria imekuwa ni muhimu kwa mataifa mengine ya nje kushirikiana katika mzozo huo. Kama ishara ya kimashirikiano, amesema Urusi na Uturuki wamekubaliana kuanzisha doria ya pamoja ili kuyakabili makundi ya itikadi kali mkoani humo. Hata hivyo hakutoa maelezo zaidi kuhusu makubaliano hayo ya kijeshi. 

Syrien Krieg | Zerstörung in Aleppo
Baadhi ya maeneo ya Idlib yanayoonekana kuharibiwa vibaya kwa vitaPicha: Getty Images/AFP/A. Watad

Erdogan ametoa mwito wa ushirikiano na Urusi katika jitihada hizo na kusema Uturuki imefanya juhudi kubwa za kuzuia mashambulizi katika baadhi ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi katika mkoa wa Idlib, karibu na mpaka wake.

''Tunafanya juhudi kubwa za kumaliza tatizo la makundi ya itikadi kali huko Idlib, na hususan ili kuzuia mashambulizi kwenye kambi ya Urusi ya Khmeimim.''

Rais wa Urusi Vladimir Putin naye akasisitizia ushirikiano baina yao katika kufanikisha juhudi hizo ambazo tayari zimeanzishwa.

''Tumekwishafanya mengi kwa pamoja, tumetoka mbali na tunajua kwamba haikuwa rahisi. Sio masuala yote yamesuluhishwa, lakini kama tutaendelea kushirikiana nina hakika tutafanikiwa.''

Mwanzoni mwa mkutano huo, Urusi iliieleza Uturuki kwamba haina mamlaka ya kuanzia ukanda salama ndani ya Syria, hadi pale itakapoomba na kupata kibali kutoka kwa rais Bashar al-Assad wa Syria, matamshi yaliyoashiria hali ya wasiwasi kwenye mkutano huo wa kilele.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani amewaeleza washirika wenzake hao kwamba anaunga mkono juhudi za kuyaondosha makundi hayo ya wanamgambo mkoani Idlib, akisema itakuwa ni kosa kuendelea kuyakumbatia, kwa kuwa tu yamebadilisha utambulisho wao.

Mataifa yote matatu yana wanajeshi wake nchini Syria, ambako wameunganisha nguvu licha ya wakati mwingine kutofautiana kimaslahi na vipaumbele.

 

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/DPAE.

Mhariri: Grace Patricia Kabogo