1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaadhimisha miaka 5 tangu kuliteka jimbo la Crimea

Zainab Aziz Mhariri:Josephat Charo
18 Machi 2019

Urusi leo inaadhimisha mwaka wa tano tangu ilipoliteka jimbo la Crimea lillilokuwa sehemu ya Ukraine na  rais Vladimir Putin anatarajiwa kuhudhuria maadhimisho hayo kwenye rasi hiyo  iliyopo kwenye bahari  nyeusi.

https://p.dw.com/p/3FEaW
Moskau Jahrestag Krim Annektion Konzert Putin Plakat
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/S. Bobylev

Rais wa Urusi Vladimir Putin leo anatazamiwa kuwasili kwenye jimbo la Crimea ili kushiriki katika  maadhimisho ya mwaka wa tano tangu nchi yake ilipoliteka jimbo hillo. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, Rais Putin atadhuhuria maadhimisho hayo kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Sevastopol.

Hatua hiyo ya Urusi ya kuliteka jimbo la Crimea mnamo mwaka 2014 ililaaniwa vikali na Ukraine na nchi za magharibi lakini ilipongezwa na Warusi wengi. Ikulu ya Urusi imesema katika taarifa kuwa kilichotokea  miaka 5 iliyopita ni  kujiunga tena kwa rasi  ya Crimea na Urusi.

Rais Putin anatarajiwa kufungua kituo kikubwa kipya cha nishati pamoja na kukutana na wanaharakati wa asasi za kiraia. Miaka 5 iliyopita rais huyo alitia saini mkataba na wawakilishi wa Crimea ili kuhalalisha jimbo hilo kuwa sehemu ya Urusi, muda mfupi tu baada ya kufanyika kura ya maoni ambayo haikutambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Nchi za magharibi pamoja na Ukraine yenyewe zinaizingatia hatua iliyochukuliwa na Urusi miaka 5 ilyopita  kuwa ni kutekwa kwa Crimea. Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Pavlo Klimkin amesema miaka yote mitano imejenga mazingira ya ugaidi dhidi ya watu wa Crimea.

Daraja linaloziunganisha Urusi na rasi ya Crimea
Daraja linaloziunganisha Urusi na rasi ya CrimeaPicha: Reuters/P. Rebrov

Uchunguzi uliofanywa mapema mwezi huu umebainisha kwamba ni asilimia 39 tu ya Warusi wanaoamini  kwamba Crimea imeleta manufaa kwa Urusi. Mnamo mwaka 2014 warusi waliounga mkono uvamizi huo  walikuwa asilimia 67. Watu hao walisema wakati huo kwamba kutekwa kwa Crimea kulileta manufaa zaidi  kuliko hasara kwa Urusi.

Kutokana na hatua ya kuliteka jimbo la Crimea Urusi iliwekewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa lakini ilimwongezea Putin umaarufu nchini mwake wakati  huo. Nchini Urusi tarehe 18 mwezi Machi imetangazwa kuwa siku ya Urusi na Crimea kuungana tena. Shughuli mbali mbali zinafanyika barabarani kuadhimsiha siku ya leo. Watu wapatao 10,000 wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho ya leo mjini Moscow na watasakata rumba la polepole la muziki wa ala unaoitwa "Sevastopol waltz."

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema suala la Crimea limeshatatuliwa daima. Msemaji wa wizara hiyo Maria Zakharova alieleza siku kadhaa zilizopita kwamba kuungana tena kwa Urusi na Crimea ni matokeo ya uchaguzi wa hiari wa watu wa rasi ya Crimea baada ya kushiriki katika kura ya maoni.

Wiki iliyopita Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya ziliiwekea Urusi vikwazo vingine kwa kuwalenga maafisa kadhaa wa Urusi na wafanyabiashara. Wizara ya mambo ya Nje ya Urusi imesema nchi hiyo itajibu vikwazo hivyo vipya lakini haikutaja ni hatua gani zitakazochukuliwa. Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema madai ya Umoja wa Ulaya kwamba Urusi imevunja sheria za kimataifa na kutumia nguvu hayalingani na ukweli uliopo.

Vyanzo: AFPE/RTRE