1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaelekeza mashambulizi yake mkoa wa Donbas

Sylvia Mwehozi
26 Mei 2022

Urusi imeishambulia zaidi ya miji 40 katika mkoa wa Donbas mashariki mwa Ukraine na kuharibu majengo kadhaa ya roshani, wakati vikosi vya Moscow vikijaribu kuwazingira askari wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/4BtJF
Ukraine Invasion Russlands Donbass
Picha: Aris Messinis/AFP/Getty Images

Baada ya kushindwa kuudhibiti mji mkuu wa Ukraine wa Kyiv au ule wa pili wa Kharkiv katika vita vyake vya miezi mitatu, Urusi sasa imeelekeza nguvu zake katika kuukamata kikamilifu mji wa Donbas kwa niaba ya wale wanaotaka kujitenga. Mkoa huo wa kiviwanda una majimbo mawili ya Luhansk na Donetsk.

Urusi imesambaza maelfu ya wanajeshi katika mkoa huo wanaofanya mashambulizi kutokea pande tatu kwa lengo la kuzingira vikosi vya Ukraine ambavyo bado vinadhibiti mji wa Sievierodonetsk na mji pacha wa Lysychansk Ofisi ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy imesema kwamba kiasi cha majengo 11 ya roshani yameharibiwa kwenye miji hiyo miwili.

Naye kiongozi wa Jamhuri ya watu wa Donetsk DPR anayeungwa mkono na Urusi Denis Pushilin ametaka operesheni ya kijeshi katika mkoa wa Donbas kuongezwa kasi, kwasababu Ukraine imezuia usambazaji wa maji katika mikoa muhimu ya kaskazini mwa mkoa huo. 

Ukraine-Krieg | Gefechte im Donbass
Askari wa Ukraine katika mkoa wa DonbasPicha: Alex Chan Tsz Yuk/SOPA Images/ZUMA Press/picture alliance

Wakati huohuo Rais Zelensky ameyakosoa vikali mataifa ya magharibi kwa kutochukua hatua za kutosha kuisaidia nchi yake kushinda vita. Katika hotuba yake ya kila siku kwa taifa, Zelenksy amesema Ukraine inahitaji zaidi msaada kamili wa silaha "bila ubaguzi na bila kikomo".

"Vikosi vya wanajeshi wa Ukraine, ujasusi watu na wale wote wanaotetea nchi wanapinga mashambulizi makali sana ya wanajeshi wa Urusi huko mashariki. Katika baadhi ya maeneo, adui ametuzidi zaidi katika suala la vifaa na idadi ya askari."

Aidha kiongozi huyo ameongeza kuwa ulimwengu haukuwa tayari "kwa ushujaa wa Ukraine", na kuitaja jumuiya ya kimataifa kwamba imezingatia sana Urusi kuliko Ukraine.

Hapo awali, waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba aliwaeleza washiriki wa jukwaa la kiuchumi mjini Davos kwamba nchi yake inahitaji mifumo kadhaa ya maroketi ili kuendana na silaha za Urusi katika mapambano ya Donbas.

Hayo yakijiri Uturuki ipo katika mazungumzo na Urusi pamoja na Ukraine ya kufungua njia kupitia nchi hiyo kwa ajili ya usafirishaji wa ngano kutoka Kyiv. Bandari za Ukraine katika bahari nyeusi zimezuiwa tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi na zaidi ya tani milioni 20 za ngano zimekwama.

Urusi na Ukraine zinachangia kwa karibu theluthi tatu ya usambazaji wa ngano duniani kote na kutatizika kwa usambazaji kumechangia kuongezeka kwa mgogoro wa chakula duniani.