1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yafanya harakati kubwa za kijeshi Arctic

Josephat Charo
16 Februari 2017

Urusi chini ya uongozi wa rais Putin inaelezwa kuwa na juhudi pana za kufanya mkakati mkubwa kabisa wa kijeshi kuwahi kushuhudiwa katika eneo la Arctic tangu kusambaratika kwa Muungano wa zamani wa Sovieti.

https://p.dw.com/p/2XhEw
Eisbrecher Jamal
Meli kwa jina Jamal ikiondoka Murmansk kuelekea kituo cha Urusi katika eneo la ArcticPicha: picture-alliance/dpa/L. Fedoseyev

Karibu miongo mitatu tangu meli ya Lenin ilipoacha kutumika na kugeuzwa kuwa meli ya makumbusho na kivutio cha wageni, Urusi kwa mara nyingine tena iko mbioni kujenga meli mpya zinazoendeshwa na nishati ya nyuklia zinazotumika katika maeneo ya maji yaliyofunikwa na theluji. Meli ya Lenin ni alama ya fahari katika bahari ya Arctic ya enzi ya muungano wa Sovieti, ambayo inapatikana hivi sasa katika mji wa Murmansk. Ni mabaki ya enzi ya vita baridi ambayo sasa ni makumbusho.

Juhudi hizi ni sehemu ya mkakati wa Urusi kuwa na udhibiti katika eneo la kaskazini la dunia huku ikipigania kuwa na ushawishi na mahasimu wake wa tangu jadi, Canada, Marekani na Norway, pamoja na China. Mahojiano yaliyofanywa na maafisa wa jeshi na wachambuzi wa masuala ya kijeshi yamebaini kuwa harakati za Urusi ni kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu kuanguka kwa muungano wa Sovieti mnamo 1991 na katika maeneo fulani utaipa Urusi uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi kuliko uliokuwa nao muungano huo.

Russland Präsident Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: picture alliance/V. Prokofyev/TASS/dpa

Utanuzi huo umeleta changamoto kubwa kifedha na kijiografia. Eneo la Arctic linakadiriwa kuwa na utajiri mkubwa zaidi wa mafuta na gesi kuliko Saudi Arabia na Urusi imeng'amua kuweka alama ya wazi ya kijeshi katika eneo hilo.

"Historia inajirudia," alisema Vladimir Blinov, afisa anayewatembeza wageni katika meli ya Lenin, iliyopewa jina la mwanaharakati wa mageuzi wa kikomunisti, Vladimir Lenin. Akizungumza na kundi la wageni walioitembelea meli hiyo Blinkov alisema, "Wakati huo katika miaka ya 1950 ilikuwa kilele cha vita baridi na Marekani ilikuwa ikiongoza katika baadhi ya maeneo. Lakini tuliwapiku wamarekani na kujenga meli ya kwanza duniani inayoendeshwa kutumia nishati ya nyuklia, Lenin. Hali leo inafanana," akasema afisa huyo.

Harakati za kijeshi zaongozeka chini ya Putin

Chini ya Putin Urusi inaharakisha kuzifungua tena kambi za jeshi la anga na rada katika visiwa vilivyo mbali kabisa katika eneo la Arctic na kujenga kambi mpya, huku ikidai kujiongezea karibu maili nusu milioni ya eneo hilo katika himaya yake. Mara kwa mara Urusi hutoa picha za wanajeshi wake wakifanya mazoezi wakiwa wamevalia mavazi meupe na wakishika bunduki.

Kwa mujibu wa makadirio ya Shirika la Jiolojia la Marekani, aneo la Arctic lina utajiri wa mafuta na gesi sawa na thamani ya mapipa bilioni 412 ya mafuta, takriban asilimia 22 ya mafuta na gesi ambayo haijagunduliwa duniani kote. Bei za chini za mafuta na vikwazo vya mataifa ya magharibi vilivyowekewa Urusi kutokana na harakati zake nchini Ukraine ina maana miradi mipya katika bahari ya Arctic kwa sasa imekwamishwa, lakini utawala wa Kremlin unacheza mchezo wa muda mrefu.

USA Präsident Donald Trump
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Inajenga meli tatu mpya zinazotumiwa katika maeneo ya maji yaliyofunikwa na theluji zinazoendeshwa kutumia nyuklia, ikiwamo meli kubwa kabisa duniani, kuimarisha idadi jumla ya meli zake 40, sita kati yao zikiwa na nyuklia. Hakuna nchi nyingine yenye meli nyingi za aina hii zinazotumiwa kusafisha njia za baharini kwa ajili ya meli za kijeshi na za kiraia.

Waziri mpya wa ulinzi wa Marekani, James Mattis, amezieleza harakati za Urusi katika eneo la Arctic kuwa uchokozi na kuahidi kuandaa mkakati madhubuti wa Marekani kuikabili Urusi. Mattis amewahi kusema "si kwa masilahi ya Marekani kuiacha sehemu yoyote ya ulimwengu kwa wengine." Hali hii inamuweka rais wa Marekani, Donald Trump, katika mtanziko, akitaka kurejesha uhusiano wa kawaida na Urusi na kushirikiana na serikali ya mjini Moscow katika kuvimaliza vita vya Syria, badala ya kutumbukia katika vita vya silaha katika eneo la Arctic.

Ongezeko la shuhguli za Urusi katika eneo la Arctic limezua wasiwasi katika maeneo mengine. Wanajeshi 300 wa Marekani walipelekwa Norway mwezi huu kuhudumu kwa kipindi cha miezi sita, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia. Na baada ya Urusi kulitwaa eneo la Crimea mwaka 2014, jumuiya ya kujihami ya NATO inafuatilia kwa karibu sana suala hili. Nchi sita wanachama wa jumuiya hiyo zilifanya luteka za kijeshi katika eneo la Arctic mwaka 2015.

Mwandishi:Josephat Charo/rtre

Mhariri:Saumu Yusuf