Urusi yaialika Taliban kwa mazungumzo
20 Oktoba 2021Urusi imeitisha hivi leo mkutano juu ya Afghanistan unaowahusisha wawakilishi wa ngazi za juu wa serikali ya Taliban na mataifa jirani, ikiwa sehemu ya juhudi za kidiplomasia zinazoashiria jinsi Moscow inavyotaka kuwa sehemu ya mustakabali wa Afghanistan katika jukwaa la kilimwengu.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, aliyafunguwa mazungumzo hayo leo akisisitiza kwamba kuunda serikali jumuishi inayoakisi maslahi ya makabila na vikundi vyote vya kisiasa nchini Afghanistan ni muhimu sana katika kupata amani ya kudumu nchini humo.
Soma pia: Marekani,Taliban kufanya mazungumzo ana kwa ana mjini Doha
Hata hivyo, waziri huyo wa mambo ya nje alielezea kutambua juhudi za Taliban kujaribu kuitulizanisha nchi licha ya wasiwasi wa makundi ya kigaidi yanayotishia usalama wa eneo zima, "Hali ya sasa nchini Afghanistan haiwezo kuitwa kwamba imeshatulia. Kuna makundi kadhaa ya kigaidi yanayojaribu kuitumilia hali iliyopo. Kwanza ni Dola la Kiislamu na al-Qaida, ambayo kwa mara nyengine yanajaribu kuja juu, yakifanya mashambulizi mabaya kabisa maeneo kadhaa ya nchi."
Putin ameonya kwamba wapiganaji wa kundi la IS wanakusanyika nchini Afghanistan
Lavrov aliwaambia wajumbe kutoka mataifa 10 zikiwemo China na Pakistan kwamba lazima wakubaliane na ukweli kwamba utawala mpya sasa upo madarakani nchini Afghanistan, akielezea masikitiko yake kwamba Marekani haikukubali kushiriki mazungumzo hayo.
Mkutano huo ni moja kati ya mikutano ya ngazi za juu ya kimataifa kuhusu Afghanistan tangu Taliban kuingia madarakani katikati ya mwezi Agosti.
Mazungumzo haya yanafanyika baada ya Rais Vladimir Putin kuonya wiki iliyopita kwamba wapiganaji wa kundi la IS wanakusanyika nchini Afghanistan kwa ajili ya kusambaza machafuko katika mataifa ya zamani ya lililokuwa shirikisho la Usovieti yanayopakana na Urusi.
Ujumbe wa Taliban kwenye mazungumzo hayo unaongozwa na Naibu Waziri Mkuu Abdul Salam Hanafi, kiongozi wa ngazi za juu wa utawala mpya wa Afghanistan aliyeongoza mazungumzo na Umoja na Ulaya na Marekani wiki iliyopita, ambayo yalifuatiwa na mazungumzo mjini Ankara kati ya maafisa wa Taliban na Uturuki.
Soma pia: Ujumbe wa Uingereza wakutana na maafisa wa Taliban
Katika mafanikio ya mikutano hiyo ni ahadi ya Umoja wa Ulaya kutoa msaada wa euro bilioni moja kukabiliana na janga la kibinaadamu linalolinyemelea taifa hilo.
Urusi imekuwa ikiwasiliana na Taliban na kuita mikutano na wawakilishi wake mara kadhaa mjini Moscow, ingawa Taliban inatambuliwa kama kundi la kigaidi nchini Urusi.
Rais Putin na maafisa wa ngazi za juu nchini Urusi wamekuwa wakipaza sauti zao juu ya masuala ya usalama nchini Afghanistan tangu Taliban kuchukuwa udhibiti na majeshi ya kigeni kujiondowa baada ya miaka 20 ya kulikalia taifa hilo la Asia ya Kati.