Urusi yatoa wito wa mazungumzo kuhusu vita vya Ukraine
7 Novemba 2024Urusi leo imetoa wito wa mazungumzo baina yake na nchi marafiki wa Ukraine ili kusitisha mashambulizi kwa raia wa Ukraine.
Haya yamesemwa na mkuu wa Baraza la Usalama la Urusi, Sergei Shoigu, aliyedai kwamba mataifa ya Magharibi yana chaguo la ama kuzungumza na Urusi kuhusiana na vita hivyo au raia wa Ukraine waendelee kutaabika.
Soma: Urusi yaionya Ufaransa fikra ya kupeleka wanajeshi Ukraine
Shoigu ameyasema haya wakati ambapo Ukraine usiku wa kuamkia leo ilikuwa inapambana kukabiliana na mkururo wa mashambulizi ya ndege zisizokuwa na rubani kutoka Urusi.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Ukraine vimeripoti kuwa mamlaka katika eneo la Donetsk zinajiandaa kutangaza uhamishaji wa lazima wa watu kutoka vijiji saba zaidi vya eneo hilo, ambavyo mwaka 2022 Urusi ilidai kwamba ni sehemu ya himaya yake.