1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yajitetea kujiimarisha kijeshi kwenye mpaka na Ukraine

10 Aprili 2021

Urusi imedai kwamba hatua yake ya kujimarisha kijeshi karibu na mpaka wa Ukraine na katika rasi iliyoinyakua kimabavu ya Crimea, ilikuwa ni sehemu ya majibu yake dhidi ya uchokozi ulioanzishwa na Kyiv.

https://p.dw.com/p/3ro4d
Russland BMP-3-Infanterie-Kampffahrzeug
Picha: Alexey Maishev/Sputnik/dpa/picture alliance

Maafisa wa Urusi wamedai jana Ijumaa kwamba hatua yake ya kujimarisha kijeshi karibu na mpaka wa Ukraine na katika rasi iliyoinyakua kimabavu ya Crimea ilikuwa ni sehemu ya majibu yake dhidi ya uchokozi ulioanzishwa na Kyiv.

Wasemaji wa ikulu ya Kremlin na wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi wamerejelea wasiwasi wa vita vya wenyewe kwa wenyewe ama hata uwezekano wa shambulizi la mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa jamii ya wachache wanaozungumza Kirusi waishio Ukraine pamoja na uchokozi unaofanywa na Kyiv kama mambo yatakayochochea hatua zisizotarajiwa za kijeshi.

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alikuwa akiwajibu kansela wa Ujerumani Angela Merkel na msemaji wa ikulu ya White House ya Marekani Jen Psaki.

Walipozungumza kwa njia ya simu siku ya Alhamisi, Merkel alimtolea mwito rais Vladimir Putin wa Urusi kuwaondoa wanajeshi ili kufikia lengo la kupunguza wasiwasi kwenye eneo hilo la mpaka.

Russland Kampfpanzer T-72B3 Militärparade
Ukraine na mataifa ya magharibi yamekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na kujiimarisha kijeshi kwa UrusiPicha: Alexey Maishev/Sputnik/dpa/picture alliance

Ni nini kinacholeta wasiwasi kwa Ukraine na magharibi?

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Anthony Blinken pia alifanya mazungumzo na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas na Jean-Yves Le Drian wa Ufaransa Ijumaa hii, ikiwa ni kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Kwenye mazungumzo ya simu kwa nyakati tofauti, Blinken na Le Drian "walijadiliana kwamba Urusi inatakiwa kuacha mara moja maneno yake makali na yasiyo ya uwajibikaji, kujiimarisha kijeshi katika rasi iliyoinyakua kimabavu ya Crimea na katika eneo la mpaka na Ukraine," amesema msemaji wa wizara hiyo Ned Price, wakati Blinken na Maas walisisitiza "umuhimu wa kuisaidia Ukraine dhidi ya uchokozi wa Urusi."

Alipoulizwa kuhusu matamshi ambayo Dmitry Kozak-mkuu wa mazungumzo wa Urusi, katika makubaliano na Ukraine- aliyeelezea wasiwasi wa mauaji ya halaiki kama yale ya Srebrenica mnamo mwaka 1995 wakati wa vita na Bosnia, msemaji wa Kremlin Peskov alidai kwamba maneno hayo matupu ya mzalendo nchini ukraine yalikuwa yalichochea chuki dhidi ya watu wanaozungumza Kirusi wanaoishi eneo la mashariki.

Maafisa wa Ukraine na mataifa ya magharibi wameelezea wasiwasi wao katika wiki za karibuni kuhusiana na kuongezeka kwa ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano katika jimbo la Donbass, ambako kwa kiasi kikubwa kunakabiliwa na  mapigano tangu mwaka 2014. Zaidi ya watu 14,000 wamefariki dunia kutokana na mzozo huo na juhudi za kusuluhisha bado hazijazaa matunda.

Kwa nini Marekani na Uturuki zinahusika?

Türkei Istanbul 2021 | USS Thomas Hudner, U.S. Navy
Manowari ya kivita ya Marekani ikielekea kwenye Bahari Nyeusi, mjini Instanbul UturukiPicha: Murad Sezer/REUTERS

Marekani imeitaarifu Uturuki kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni kwamba itapeleka manowari mbili za kivita wiki ijayo kuangazia hali ya mambo. Manowari hizo za Marekani zitaingia kwenye eneo hilo Aprili 14-15 na kuondoka Mei 5 kulingana na masharti yaliyomo kwenye Mkataba wa Montreux wa mwaka 1936.

Rais wa Urusi Vladimir Putin Ijumaa hii amemuomba rais wa Urusi Recep Tayyip Erdogan kuuendeleza mkataba huo wa Montreux. Ombi hilo halionyeshi kama huenda likaleta kizuizi chochote kwenye safari ya manowari hizo za Marekani wiki ijayo, ingawa linaweza kuwa na athari katika siku za usoni, wakati Marekani itakapohitaji kutumia Bahari Nyeusi.

Hatua ya Marekani ya kupeleka manowari si ya kawaida sana, na Moscow imekuwa ikibugudhiwa kwa muda mrefu na hatua za majaribio za Ukraine katika kuimarisha amhusiano na Magharibi tangu mabadiliko ya serikali ya mwaka 2014, lakini pia hamu yake ya kutaka kujiunga na muungano wa kijeshi wa NATO.

Siku ya Ijumaa, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi Maria Zarakhova ameonya kwamba kuviunga mkono vikosi vya Jumuiya ya kujihami ya NATO, "sio tu kutapelekea kusambaa kwa sintofahamu katika eneo la kusinimashariki, bali pia kutasababisha athari ambazo hazikutarajiwa nchini Ukraine.