1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yalaani kutoalikwa mazishi ya Malkia Elizabeth

16 Septemba 2022

Viongozi wa mataifa mbalimbali duniani wanahudhuria maziko ya Malkia Elizabeth yanayofanyika Jumatatu, lakini Urusi haitahudhuria kwa kutokualikwa, ikisema ni dalili ya ukosefu wa maadili kwa upande wa wenye msiba huo.

https://p.dw.com/p/4Gxie
Großbritannien London | Trauer um Queen Elizabeth II
Picha: Nathan Denette/The Canadian Press/AP/picture alliance

Maraisi, mawaziri wakuu na wafalme kutoka kote ullimwenguni watasafiri kuelekea London mwishoni mwa wiki kutowa heshima zao za mwisho kwa Malkia Ellizabeth na kuhudhuria mapokezi katika Kasri la Buckingham yatakayoongozwa na Mfalme Charles siku moja kabla ya mazishi yenyewe.

Miongoni mwa viongozi wa mataifa makubwa wanaohudhuria mazishi hayo ni Rais Joe Biden wa Marekani na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron. 

Wageni wote wataombwa kukusanyika katika Hospitali Kuu na baadaye kusafirishwa kwa makundi kuelekea Westminister Abbey, kutoa heshima zao za mwisho mbele ya mwili ya Malkia utakaokuwa umelazwa kwenye ukumbi wa bunge kabla ya mazishi.

Mialiko 1,000 ya kuhudhuria maziko hayo imetumwa kwa takribani wakuu wa nchi zote duniani isipokuwa Syria, Venezuela, Afghanistan, Urusi, Belarus na Myanmar.

Waingereza wauaga mwili wa Malkia Elisabeth II

Ambapo sababu za kutoalikwa Syria na Venezuela ni kutokuwa kwao na mahusiano ya kibalozi na Uingereza kwa sasa, Afghanistan haikupewa mualiko kutokana na hali yake ya kisiasa, na Urusi na Belarus zimenyimwa mualiko kwa sababu ya uvamizi dhidi ya Ukraine.

Urusi yalaani

Vladimir Putin
Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: Gavriil Grigorov/Sputnik/Kremlin Poo//AP/picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Urusi imelaani vikali hatua hiyo ya kutokualikwa ikisema ni "kiwango cha chini kabisa cha ukosefu wa maadili".

Msemaji wake wa wizara ya mambo ya kigeni, Maria Zakharova, amesema hivi leo kwamba kuutumia msiba wa kitaifa kulipiza kisasi siasa za kilimwengu ni kupotoka, akiilaumu Uingereza kwa kuegemea kile alichokiita "upande wa Wanazi" na wasaidizi wao wa Ukraine.

"Lazima tuseme kwamba mfano wa Malkia Elizabeth wa Pili, ambaye alikuwa nguvu madhubuti ya kuunganisha nchi na hakuingilia mambo ya siasa wakati wa utawala wake kama suala la kimaadili, haukuizuwia London kutoa kauli za kugawanya watu kwa kuendeleza maslahi ya uroho wake." Alisema Zakharova.

China kuhudhuria

China Präsident Xi Jinping
Rais Xi Jinping wa China.Picha: Ng Han Guan/AP Photo/picture alliance

Hata hivyo, China, ambayo nayo ina tafauti zake kubwa na nyingi na ulimwengu wa Magharibi, imealikwa kuhudhuria kwenye mazishi hayo, hatua ambayo imekosolewa vikali na kundi la wabunge wa Uingereza ambao wamewekewa vikwazo na China. 

Wabunge hao sasa wanataka wawakilishi wa China wazuiwe kuingia kwenye jengo la bunge, ambako mwili waMalkia Elizabeth utakuwa umewekwa kuagwa. 

Makamu Rais wa China, Wang Qishan, anatazamiwa kuiwakilisha nchi yake kwenye mazishi hayo siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza.

China ilichukuwa hatua kali dhidi ya baadhi ya wabunge wa Uingereza kwa kile ilichosema ni kuingilia kwao masuala ya ndani ya China, hasa siasa za Hong Kong na hatua ya bunge hilo kupiga kura ya kuviita vitendo vya serikali ya China dhidi ya jamii ya Waislamu wa Uighur jimboni Xinjiang kuwa ni mauaji ya kimbari.