Urusi yasema Prigozhin hatashitakiwa
27 Juni 2023Shirika la Usalama la Urusi (FSB) limesema uchunguzi wake ulibaini kuwa wale waliohusika katika uasi walisitisha maelekezo ya kufanya uhalifu huo.
Hii ni baada ya mwishoni mwa juma serikali kutoa ahadi ya kutomshitaki Prigozhin na wapiganaji wake baada ya kusitisha uasi wa Jumamosi iliyopita, ingawa Rais Vladimir Putin aliwapaichka wapiganaji hao jina la waasi.
Shitaka la kuanzisha uasi wa kutumia silaha lina adhabu ya hadi miaka 20 jela.
Hadi kufikia Jumanne (Juni 27) mahali alipo Prigozhin palikuwa pamesalia kuwa siri.
Serikali ya Urusi ilisema kiongozi huyo wa kundi la Wagner angelihamishwa taifa jirani la Belarus, ingawa si yeye wala mamlaka ya Belarus waliothibitisha hilo.
Pongezi za Rais Zelensky kwa wapiganaji
Katika uwanja wa mapambano, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alisema mapambano ya majuma kadhaa yenye lengo la kuyadhibiti tena maeneo yaliyochukuliwa na Urusi yanaendelea kwa mafanikio.
"Leo hii katika maeneo ya mapambano, mikoa ya Donetsk na Zaporizhzhia, wanajeshi wetu wako vyema katika maeneo ya makabiliano. Kwa hivyo nina furaha. Nawatakia wapambanaji siku nyingine zaidi kama hizi. Hongereni sana!" Alisema kiongozi huyo wakati akiwa kwenye treni kutokea mstari wa mbele wa mapambano.
Urusi yawanyonga watu 77
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Urusi imewanyonga watu 77 waliokuwa wakishikiliwa kiholela wakati wa vita vyake nchini Ukraine.
Tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake Februari 2022, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kufuatilia Haki za Kibinadamu nchini Ukraine umerekodi visa 864 vya kuwekwa kizuizini kiholela vinavyofanywa na Urusi, vingi vikiwa vya utoeshwaji wa watu.
Kiongozi wa ujumbe huo, Matilda Bogner alisema kati ya hao 77 wanaume walikuwa 72 na wanawake watano, ambapo wafungwa wawili wa kiume walikufa kutokana na mateso na kunyimwa huduma za matibabu.
Soma zaidi:Urusi yahofiwa kutoongeza makubaliano ya ngano ya Ukraine
Matokeo ya ripoti hiyo yalitokana na mahojiano 1,136 na waathiriwa, mashahidi na wengine, pamoja na kutembelea maeneo 274 ya vizuizini yanayoendeshwa na mamlaka ya Ukraine.
Kwa ujumla, ripoti hiyo ilinakili zaidi ya kesi 900 za kuwekwa kizuizini kiholela kwa raia, wakiwemo watoto, na wazee.
Vyanzo: AFP/DPA