Urusi yadai kusonga mbele Ukraine
2 Mei 2024Hayo yanajiri muda mfupi baada ya Ukraine nayo kudai kuwa Moscow ilifanya shambulio la kombora mjini Odesa na kuwajeruhi watu wanne.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema leo Alhamisi kuwa wanajeshi wake wamefanikiwa kuliteka eneo la Berdychi lililo mashariki mwa Ukraine. Taarifa ya wizara hiyo imetolewa kupitia shirika la habari la Interfax wakati Urusi ikiharakisha juhudi zake za kusonga mbele dhidi ya Ukraine kabla ya kuwasili kwa silaha kutoka Marekani.
Kauli ya wizara ya ulinzi ya Urusi imeeleza kuwa sasa vikosi vyake vimelikomboa kikamilifu eneo la Berdychi. Hayo yanajiri wakati mamlaka katika mji wa Odesa nchini Ukraine zikiripoti leo kuwa shambulio la kombora lililofanywa na Urusi katika mji huo ulio kusini magharibi limewajeruhi watu 13.
Soma zaidi: Urusi yashambulia kiwanda cha bidhaa za kilimo kusini mwa mkoa wa Odesa nchini Ukraine
Shambulio hilo la tatu mfululizo ndani ya wiki moja linafanana na jingine lililofanywa katikati ya wiki hii lililowaua watu 8.Meya wa Odesa Gennadiy Trukhanov ametoa taarifa kuhusu shambulio hilo mapema leo kupitia ukurasa wake wa Telegram.
Kwa upande wake Gavana wa Odesa amelizungumzia tukio hilo pia kupitia Telegram na kuongeza kuwa shambulio hilo limesababisha pia uharibifu wa miundombinu ya raia likiwemo ghala la posta.
Katika tukio jingine la hivi karibuni, Gavana wa mkoa wa Kharkiv, Oleh Synehubov amesema Urusi imeishambulia kwa mabomu miundombinu ya wananchi na makazi ya watu katika eneo hilo na kuwajeruhi watu saba, sita kati yao wakiwa ni watoto.
Kharkiv iliyo kilometa 30 kutoka mpakani na Urusi imekuwa ikilengwa na mashambulizi ya Urusi mara kwa mara.
Urusi yakanusha tuhuma za kutumia silaha za kemikali
Wakati huo huo, ikulu ya Kremlin kupitia msemaji wake Dmitry Peskov imekanusha madai ya Marekani kuwa wanajeshi wake walitumia silaha za kemikali dhidi ya Ukraine.
Peskov amesema kuwa kama kawaida kauli kama hizo hazina msingi wowote. Ameongeza kuwa Urusi imekuwa na itaendelea kutimiza wajibu wake katika sheria ya kimataifa kuhusu mkataba wa marufuku ya matumizi ya silaha za kemikali.
Soma zaidi: Biden adai Urusi inakusudia kutumia silaha za kemikali
Urusi imekanusha madai hayo baada ya Marekani kudai siku ya Alhamisi kuwa wanajeshi wa Urusi walikiuka marufuku ya umoja wa mataifa dhidi ya matumizi ya silaha za kemikali kwa kutumia kemikali aina ya chloropicrin dhidi ya wanajeshi wa Ukraine.