Urusi yazuwiya ugavi wa gesi kwa Ukraine
16 Juni 2014Ukraine iliandaa mazungumzo hayo kama juhudi za mwisho kwa matumaini ya kuzuwiya uhaba wa nishati usiwaongezee matatizo viongozi wake wenye kuelemea mataifa ya magharibi wakati wakikabiliana na uasi wa miezi miwili wa kutaka kujitenga unaotishia kuwepo uhai wa taifa hilo lenyewe ambalo ni jimbo la zamani la muungano wa Kisovieti.
Serikali ya Ukraine ilipata pigo jengine leo hii wakati waasi kadhaa wenye bunduki za Kalashnikov walipolinyakuwa jengo la benki kuu katika mji ulio ngome kuu ya waasi wa Donetsk katika harakati za kudhibiti mali zake.
Kampuni kubwa ya gesi ya Urusi Gazprom imesema imeurudisha kwa Ukraine utaratibu wa kulipwa na mapema hatua ambayo moja kwa moja inazuwiya shehena yote ya nishati hiyo kuanzia Jumatatu (16.06.2014) kwa sababu serikali ya Ukraine haikuwasilisha fedha zozote zile na mapema kwa ajili kupatiwa gesi ya kipindi cha usoni kutoka Urusi.
Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk ameita hatua hiyo ya kuzuwiya usambazaji kuwa ni awamu nyengine ya uvamizi wa Urusi dhidi ya taifa la Ukraine.
Kutibuka kwa ugavi Ulaya
Kampuni ya Gasprom imesema imeijulisha Ulaya juu ya uwezekano wa kutibuka kwa ugavi wa gesi na imefunguwa kesi ya madai ya dola bilioni 4.5 dhidi ya Ukraine katika mahakama ya upatanishi ilioko Stockholm Sweden.
Serikali ya Ukraine nayo imejibu hatua hiyo kwa kufunguwa kesi kama hiyo ya madai katika mahakama hiyo hiyo ya Stockholm kudai kurudishiwa malipo ya ziada kwa gesi ya huko nyuma.
Wachambuzi wanasema Ukraine ina akiba ya gesi ya kutosha kuweza kutumika katika miezi hii ya majira ya joto na kwamba hakuna bughudha itakayotokea Ulaya kutokana na ugavi wa gesi hiyo hadi msimu wa kuhitaji vipasha joto utakapoanza.
Vita vya tatu vya gesi
Vita hivyo vya tatu vya gesi kati ya Urusi na Ukraine kushuhudiwa tokea mwaka 2006 vilianza wakati Urusi ilipoongeza karibu maradufu bei zake kutokana na uasi wa majira ya baridi uliosababisha maafa na kukomesha ushawishi wa kihistoria wa serikali ya Urusi kwa Ukraine kwa mara ya kwanza kabisa.
Ukraine inapata nusu ya gesi yake kutoka Urusi na husafirisha nje asilimia 15 ya nishati hiyo inayotumika barani Ulaya jambo ambalo limemfanya Kamishna wa Nishati wa Umoja wa Ulaya Guenther Oettinger kuingilia kati kwa dharura kujaribu kuutatuwa mfarakano huo.
Taifa hilo lenye watu milioni 46 lilitumia sehemu ya shehena ya gesi ya Urusi iliopangwa kupelekwa Ulaya kufidia uhaba wakati wa mizozo ya gesi iliopita.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman