Urusi,Iran na Uturuki zatafautiana juu ya Syria
7 Septemba 2018Mgogoro wa Syria na hasa katika jimbo la Idlib unazidi kutia mashaka.Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan ametowa mwito wa kusitishwa vita katika eneo hilo la Kaskazini Mashariki mwa Syria akisema mashambulizi yanayotarajiwa kufanywa na vikosi vya serikali dhidi ya waasi katika eneo hilo huenda yakasababisha maangamizi ya watu wengi.Lakini wito wake huo umepingwa na rais wa Urusi Vladmir Putin na Iran.
Rais Putin anasema serikali yake inapinga usitishaji mapigano Idlib na kiongozi wa Iran Hassan Rouhani anasema Serikali ya Syria lazima iyakomboe maeneo yake yote.Putin amesisitiza kwa kusema hivi:
'Makundi yaliyobakia ya wenye siasa kali sasa yamejikusanya katika eneo lisilokuwa na vita katika jimbo la Idlib. Magaidi hawa wanajaribu kuuhujumu utawala wa amani''
Putin,mshirika mkubwa wa Assad ametowa onyo kwa wanamgambo walioko Idlib,kundi la Nusra Front na IS wajisalimishe wakati mwenzake wa Iran Hassan Rouhani akiiunga mkono moja kwa moja hoja ya kuendelea kwa vita vya kuwang'oa wanamgambo.
Mapigano dhidi ya magaidi katika mkoa wa Idlib hayawezi kuepukika ni sehemu ya harakati za kuleta amani na uthabiti nchini Syria.Lakini vita hivi havipaswi kuwadhuru raia.''
Putin,Rouhani na Erdogan nchi zao ni wahusika muhimu wa kigeni katika mgogoro huu wa Syria wameonesha misimamo ya kutafautiana katika mkutano wao wa kilele mjini Tehran ambao kimsingi ulikusudia kutafuta njia ya kuumaliza mgogoro huu wa kutisha. Erdogan ametowa mwito vita visitishwe kabisa na pande zote mbili.
Wimbi la wahamiaji limeanza tena na mahala wanakokwenda siku zote ni mpakani mwa Uturuki. Hivi sasa wanaelekea kwenye mipaka yetu. Hapa lazima tufikie usitishwaji wa mapigano,tuchukue hatua dhidi ya makundi ya kigaidi kwa ushirikiano wa pamoja wa maafisa wetu husika.''
Hali katika jimbo hilo ambalo ni ngome pekee kubwa iliyobakia ya wanamgambo ni suala la kipaumbele katika wakati ambapo vikosi vya serikali ya rais Bashar al Assad vinavyoungwa mkono na Urusi pamoja na Iran vinajiandaa kwa kile ambacho huenda kikawa ni mapigano makubwa ya kufa na kupona.
UN Yatahadharisha
Umoja wa Mataifa umeshaonya kwamba mapambano hayo huenda yakasababisha janga kubwa la kibinadamu lakini pamoja na viongozi kuwepo Tehran wakijadiliana suala hilo huko Syria taarifa zinazotolewa na kundi linaofuatilia masuala ya haki za binadamu zinasema ndege za kivita za Urusi na Syria zimeshayashambulia maeneo kadhaa ya jimbo hilo la Idlib.Uturuki ambayo pia ina wanajeshi ndani ya Syria inapingana na msimamo wa Iran na Urusi na Syria yenyewe.
Katika kauli yake ya ufunguzi wa mkutano wa leo Erdogan amesisitiza mwito wake wa kumtaka Putin na Rouhani kuridhia kusitisha vita katika jimbo la Idlib akisema makubaliano kama hayo yanaweza kuwa ushindi wa mkutano wao huo wa kilele na juu ya hilo Erdogan ameongeza kusema kwamba hatua za pamoja zitakazochukuliwa zitakuwa na kuzuia wakimbizi zaidi kutoka Syria.Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano imeeleza kwamba nchi hizo tatu, Iran Urusi na Uturuki zimekubaliana kukutana tena juu ya Syria huko Urusi.
Mwandishi:Saumu Mwasimba/AFPE/APE/Reuters
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman