1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

USAID: Usambazaji misaada mkoani Tigray bado changamoto

Sylvia Mwehozi
5 Agosti 2021

Mkuu wa shirika la misaada la Marekani-USAID Samantha Power ameelezea wasiwasi juu ya kauli za kudhalilisha zinazotumiwa na viongozi wa Ethiopia katikakati mwa mgogoro uliodumu kwa miezi tisa sasa katika mkoa wa Tigray

https://p.dw.com/p/3yZXm
 Äthiopien I Hungerkrise in Tigray
Picha: Eduardo Soteras/AFP

Mkuu huyo wa USAID Samantha Power alizungumza Jumatano na waandishi wa habari baada ya kuishinikiza serikali ya Ethiopia kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu katika mkoa wa Tigray, ambako maelfu ya raia wanakabiliwa na njaa katika mgogoro mbaya ulimwenguni wa njaa. Samantha amesema ni asilimia 10 pekee ya misaada iliyokusudiwa ambayo imeweza kufika katika mkoa huo tangu katikati mwa mwezi uliopita.

"Ndani ya siku mbili zilizopita magari 153 yenye misaada yaliweza kuingia Tigray. Kwahiyo katika kipindi cha kati ya Julai na Agosti 2, kulingana na Umoja wa Mataifa, kile kilichohitajika kilikuwa ni magari 1,500 na idadi ya magari yaliyoweza kupita ni 153 tu sawa na asilimia 10."

Serikali ya Ethiopia katika wiki za hivi karibuni imeyashutumu mashirika ya kutoa misaada kwa kuyaunga mkono majeshi ya Tigray, lakini hata hivyo haikutoa ushahidi na tayariimesitisha shughuli za mashirika mawili ya kimataifa ya kiutu wakati ikilituhumu shirika la madaktari wasio na mipaka na baraza la wakimbizi la Norway kwa "kusambaza taarifa za uongo".

Samanta Power an der Central American University in San Salvador
Samantha Power mkuu wa shirika la misaada la Marekani USAIDPicha: Jose Cabezas/REUTERS

Kulingana na Power, "mahitaji ya kibinadamu yanakuwa makali kila siku" mkoani Tigray, ambako zaidi ya watu milioni tano wanahitaji usaidizi baada ya vikosi vya Ethiopia na washirika wake wanaopambana na wapiganaji wa mkoa huo, kutuhumiwa kupora na kuharibu misaada ya chakula.

Hadi sasa Tigray haina mawasiliano na ulimwengu wa nje, kutokana na kwamba mawasiliano yamekuwa chini na ni barabara  moja tu inayotumika kwa ajili ya ujumbe wa kusambaza misaada, ambao mara nyingi hukabiliwa na vizuizi na ukaguzi.

Wakati mataifa ya magharibi yakijaribu kutafuta uwezekano wa njia nyingine ya kusambaza misaada kutokea nchi jirani ya Sudan hadi Magharibi mwa Tigray, mkuu wa tume ya taifa ya udhibiti wa majanga ya Ethiopia, wiki hii amekataa wazo hilo.

Power ametaka usitishaji haraka wa mapiganao na kuanzishwa majadliano. Lakini nafasi ya mazungumzo inaonekana kuwa finyu kutokana na kwamba serikali ya Ethiopia imevitangaza vikosi vya Tigray kuwa kundi la kigaidi.

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken alizungumza na waziri mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok juu ya "kuongezeka kwa makabiliano ya silaha katika mikoa ya Amhara na Afar nchini Ethiopia, kuzorota kwa hali ya kibinadamu katika mkoa wa Tigray na ripoti za vikosi vya Eritrea kuingia tena Ethiopia, masuala ambayo yanaathiri utulivu wa kikanda".