Usalama mdogo wakwaza shughuli za uokoaji Haiti.
15 Januari 2010Licha ya huduma mbalimbali za uokoaji kuanza kutolewa na Jumuia ya kimataifa, juhudi hizo zimeelezwa kukwamishwa na usalama mdogo uliopo kwa sasa, hali ambayo inawalazimu waokoaji hao kusimamisha shughuli zao wakati giza linapoingia.
Kamanda wa kikosi cha Uokoaji na Mkuu wa kikosi kinachohusika na ulinzi wa raia katika Jamhuri ya Dominica ambaye kwa sasa yuko nchini humo kwa shughuli za uokoaji, anasema tatizo kubwa linalowakabili kwa sasa ni kutokuwepo na usalama, na kwamba leo wamefanya kazi kwa shida katika baadhi ya maeneo kutokana na magari yao kuvamiwa jana.
Anasema kumekuwa na vitendo vya wizi vinavyofanywa na watu wenye silaha, kutokana na kwamba nchi hiyo ni masikini na watu wamekata tamaa ya maisha, na ukizingatia kwamba wao hawana silaha zozote za kujilinda.
Vikosi vya Uokoaji vya kimataifa vyawasili Haiti: Vikosi vya ukoaji kutoka Jamhuri ya Dominika, Venezuela, Marekani Ufaransa na Bolivia ni miongoni mwa vikosi vya kwanza kuwasilini nchini humo kusaidia kuwafukua makumi kwa maelfu ya Wahaiti waliofukiwa na vifusi katika mji mkuu wa nchi hiyo Port au Prince, baada ya tetemeko kubwa la ardhi lenye kipimo cha 7.0 kukumbwa nchi hiyo.
Vikwazo vingine katika kusaidia watu hao waliokumbwa na maafa ni uhaba wa hospitali zinazotoa hudumai, kutokan ana kwamba nyingi ziliharibiwa na tetemeko hilo, tatizo la mawasiliano.
Jumla ya watu milioni 3.5 wanaishi katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo la ardhi, ambapo habari zinasema pia mawaziri na viongozi kadhaa wa kisiasa ni miongomi mwa waliokumbwa na maafa hayo.
Miongoni mwa mawaziri waliokufa kutokana na tetemeko hilo ni waziri wa sheria Paul Denis na mwanasiasa wa upinzani nchini humo Michel Gaillard.
Kutokana na hali ilivyo nchini Marekani tayari imeshawaondoa raia wake waliopata madhara katika janga hilo na kusema kwanza inatanguliza usalama wa raia wake kwanza.
Rais wa nchi hiyo Barack Obama pia alitaka kisiwa hiko kipewe umuhimu zaidi hususan katika kipindi hiki.
Wakati huohuo mkutano wa kimataifa wa kuijenga upya Haiti baada ya janga hilo la tetemeko la ardhi unatarajiwa kufanyika mwezi Machi.
Hata hivyo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Bernard Kouchner hakueleza mkutano huo utafanyikia katika nchi ipi.
Nao raia wa Ufaransa wapatao 60 bado hawajulikani walipio, kati ya raia elfu 1 na mia tano waishio katika nchi hiyo.
Rais wa zamani wa nchi hiyo anayeishi uhamishoni ataka kurudi nyumbani, kusaidia kuijenga upya nchi yake: Katika hatua nyingine Rais wa zamani wa nchi hiyo Jean Bertrand Aristide, ambaye anaishi uhamishoni nchini Afrika kusini tokea mwaka 2004, amearifu kuwa yuko tayari kurudi kusaidia kuijenga upya nchi yake kutokana na mathara hayo ya tetemeko kubwa la ardhi.
Mwandishi : Halima Nyanza(afp)
Mhariri:Aboubakary Liongo