Usalama waimarishwa katika London Marathon
19 Aprili 2013Milipuko hiyo miwili ambayo iliwauwa watu watatu na kuwajeruhi wengi zaidi ya 180 mjini Boston Jumatatu wiki hii, imewalazimu waandalizi wa mbio za London kuimarisha mikakati ya usalama katika jitihada za kuwapa matumaini wanariadha pamoja na takribani watazamaji nusu milioni watakaojitokeza kushangilia mitaani.
Polisi zaidi watafanya doria katika barabara itakayotumia kwa mbio hizo. Serikali ya Uingereza imeahidi kufanya kila iwezalo katika juhudi za kuhakikisha usalama wa wote watakaoshiriki tamasha hilo maarufu. Wanariadha watavaa vitambaa vyeusi, wakati waandalizi wakisema kuwa euro mbili, na senti thelathini kwa kila mwanariadha atakayemaliza mbio hzio zitatolewa kugharamia waathiriwa wa mashambulizi ya Boston.
Kutakuwa na majina makubwa katika mbio hizo pia, ambapo wakenya wote watatu walioshinda medali za mbio za marathon katika mashindano ya Olimpiki London mwaka jana watajitosa tena barabarani, pamoja na anayeshikilia rekodi ya ulimwengu mkenya Patrick Makau.
Nyota wa Olimpiki Muingereza Mo Farah, ambaye aliwika katika mbio za mita 5,000 na 10,000 katika michezo ya 2012, pia atakuwa uwanjani ijapokuwa atatimka tu mbio za nusu marathon wakati akijiandaa kushiriki katika marathon kamili.
Bingwa wa ulimwengu wa mbio za marathon Mkenya Edna Kiplagat anasema huu sasa ni wakati wa kufurahia ushindi jijini London baada ya kufanya vibaya katika mashindano ya Olimpiki. Yeye ni mmoja wa kina dada wanaopigiwa upatu kushinda mbio za kesho baada ya kumaliza wa watatu katika mbio za mwaka 2011 na wa pili katika mwaka wa 2012, zote nyuma ya mshindi Mary Keittany ambaye hatoshiriki mbio za mwaka huu.
Schürrle kuhamia Chelsea?
Klabu ya Bayer Leverkusen imefanya mazungumzo na klabu ya Chelsea ya England kuhusiana na uwezekano wa uhamisho wa mshambuliaji wake mwenye umri wa miaka 22 Andre Schürlle. Hata hivyo klabu hiyo imekanusha kuwa mkataba huo unakaribia kukamilishwa. Msemaji wa Leverkusen Meinolf Sprin amewaambia waandishi habari kuwa mkurugenzi wa spoti Rudi Voeller amekuwa jijini London Alhamisi wiki hii. Schürlle ambaye anachezea timu ya taifa ya Ujerumani ni mchezaji matata katika Bundesliga na amekuwa akihusishwa na uhamisho wa klabu ya Chelsea tangu mwaka jana.
Bayern Munich wanalenga kuweka rekodi zaidi wakati wakijiandaa kwa mchuwano wa nusu fainali dhidi ya Barcelona, Borussia Dortmund pia wanalenga kupata ushindi katika Bundesliga, kabla ya kibarua chao dhidi ya Real Madrid. Bayern ambao wanacheza ugenini dhidi ya Hanover, tayari wameshinda taji la ligi zikiwa zimesalia mechi sita msimu kukimilika, na wakawazaba Wolfsburg magoli sita kwa moja katikati ya wiki na kujikatia tikiti ya fainali ya kombe la Shirikisho – DFB Pokal, katika jitihada zao za kunyakua mataji matatu.
Nambari mbili Dortmund wamewaalika Mainz 05 na huenda wakapata kibali cha moja kwa moja cha kucheza Champions League msimu ujao kama wataendelea kushinda hadi mwisho. Timu zote zinawaza tu kuhusu mechi zao za wiki ijayo wakati wakufunzi Jupp Heynckes na Jurgen Klopp wakifanya mabadiliko machache ili kuwapumzisha wachezaji wao. Katika chini ya msururu wa ligi, kushushwa daraja kwa Greuther Fürth huenda kukakamilishwa kama watashindwa na Nuremberg kesho Jumapili. Hoffenheim wako katika nafasi ya pili kutoka nyuma wakati Augsburg wanafukuzana na Dusseldorf na Werder Bremen. Hivyo Bayer Leverkusen wanakutana na Hoffenheim, SV Hamburg dhidi ya Fortuna Dusseldorf nao Frankfurt watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya Schalke leo Jumamosi. Mchuwano mwingine wa leo ni kati ya Bremen na Wolfsburg na kisha kesho Jumapili Stuttgart watafunga kazi na Freiburg.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/Reuters/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef