1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ushindi wa Rais Putin wazua hisia mseto duniani

18 Machi 2024

Marafiki na washirika wa rais wa Urusi Vladimir Putin, wameendelea kumpongeza baada ya kuchaguliwa kwa kishindo kupitia uchaguzi wa rais, lakini viongozi wa Magharibi wameukosoa uchaguzi huo waliosema haukuwa halali.

https://p.dw.com/p/4dqLN
Urusi | Uchaguzi 2024
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Maxim Shemetov/REUTERS

China ndio iliyokuwa ya kwanza kumpongeza rais Putin, ikisema nchi hizo mbili ni majirani wakubwa na washirika wakubwa wa kimkakati katika kipindi hiki kipya. Msemaji wa wizara ya kigeni ya Beijing Lin Jian, amesema marais wa mataifa hayo mawili Xi Jinping na Vladimir Putin, wataendelea kushirikiana katika nyanja mbali mbali.

Rais wa Bosnia Milorad Dodik amesema watu wake wameukaribisha kwa furaha ushindi wa Putin, kwasababu wanamuona kama mtu wa busara na rafiki wanaeweza kumtegemea, huku rais wa Venezuela Nicholas Maduro akimuelezea Putin kama ndugu yake mkubwa aliyeshinda kwa kishindo.

Putin aweka rekodi kwenye matokeo ya uchaguzi Urusi

Hata hivyo Ukraine bila shaka haikufurahishwa na ushindi wa Putin. Rais wake Volodymyr Zelensky kwanza ameuelezea uchaguzi kutokuwa halali, kisha akaenda mbali zaidi kusema Putin amelewa madaraka na atafanya kila mbinu ya kuendelea kuongoza milele.

"Kila mtu duniani anaelewa kwaba, huyu mtu kama hiytoria inavyoonesha, amekuwa na uraibu wa madaraka, na anafanya kila anachoweza kuongoza milele. Hakuna uovu asioweza kufanya ili kuendelea kubakia madarakani na hakuna mtu duniani aliyesalama kufuatia hili. Nashukuru kila taifa, kila kiongozi na mashirika yote ya kimataifa yanayoendelea kuiona hali kama ilivyo Urusi," alisema rais Zelensky.

Nchi za Magharibi zimedai uchaguzi wa Urusi haukuwa wa huru na haki

Uchaguzi Urusi - 2024
Watu milioni 76 wamempigia kura Putin baada ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa na kuumpa ushindi wa asilimia 87.54 ya kura.Picha: Stringer/AFP

Ujerumani, Uingereza, Italia, Jamhuri ya Czech pamoja na shirika la usalama na ushirikiano barani  Ulaya OSCE, zimesema uchaguzi uliofanyika haukuwa huru wala wa  haki na uliwanyima raia wa Urusi, nafasi huru ya kumchagua wanaemtaka. Zimesema uchaguzi huu pia umeonyesha namna utawala unavyoyakandamiza mashirika ya kiraia, vyombo vya habari na Upinzani.

Lakini Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Urusi Ella Pamfilova, amesema asilimia 77.44 ya watu walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi huu wa Urais uliomalizika hapo jana, akisema hii ni rekodi kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa baada ya muungano wa kisovieti kuvunjika. Pamfilova ameongeza kuwa hii pia imeonyesha namna nchi nzima imeungana na rais Putin aliyeiongoza nchi hiyo kwa muda mrefu. Ella Pamfilova amesema takriban watu milioni 76 wamempigia kura Putin baada ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa na kuumpa Putin ushindi wa asilimia 87.54 ya kura.

Urusi inafanya uchaguzi katikati ya vita na Ukraine

Akizungumza na waandishi habari mjini Moscow baada ya kutangazwa mshindi, Putin aliye na miaka 71 aliwashukuru raia wake kwa kumuunga mkono huku akitahadharisha kuwa wale wanaotaka kuikandamiza Urusi na kuiyumbisha hawakufanikiwa na hawatowahi pia kufanikiwa katika siku za usoni. Putin pia amesema mzozo kamili kati ya Urusi na Jumuiya ya kujihami NATO huenda ukatokea, hasa baada ya Putin kudai kwamba wanajeshi wa Jumuiya hiyo wamepelekwa nchini Ukraine, nchi iliyo katika mgogoro na Urusi kwa zaidi ya miaka miwili.

afp/reuters/dpa