1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usitishaji mapigano Gaza kabla ya Iddi?

24 Julai 2014

Marekani, Qatar na Uturuki zimo katika jitihada za kupatikana kwa usitishwaji mapigano ya Gaza, huku mashambulizi ya Israel yakiuwa Wapalestina saba na ikisema inahitaji muda zaidi kuwafyeka inaowaita "magaidi wa Hamas".

https://p.dw.com/p/1Chtn
Mashambulizi dhidi ya Gaza yakiendelea alfajiri ya tarehe 24 Julai 2014.
Mashambulizi dhidi ya Gaza yakiendelea alfajiri ya tarehe 24 Julai 2014.Picha: Reuters

Wapalestina hao saba wameuawa kwa mashambulizi kutokea angani na ardhini katika eneo la Khan Yunis, kusini mwa Gaza. Kiunga cha Khuzaa kilicho kwenye mpaka na Israel na wilaya ya jirani ya Abasan zimeshuhudia mapigano makali kati ya Hamas na Israel tangu siku ya Jumanne.

"Tulishangazwa kuona dari ya msikiti ikiangukia nyumba zetu. Kuna watoto wamejeruhiwa na wengine wamekufa mashahidi. Nimejeruhiwa mkono wangu. Wengi wa wale waliojeruhiwa ni watoto. Hapa hakuna wanamgambo. Nadhani dola ya kikandamizi imepagawa na imeanza kumalizia hasira zake kwa raia, lakini hawajui wakifanyacho," alisema Abu Atta Bassal, mkaazi wa kambi ya wakimbizi ya Jabalya, ambayo ni miongoni mwa maeneo yaliyoshambuliwa usiku wa kuamkia leo (Julai 24).

Ashraf al-Qudra wa idara ya huduma za dharura, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba waliouawa ni watu watano wa familia moja ya Abu Daqqa na wawili wa familia nyengine ya Najjar.

"Tumekuwa tukipokea maombi kadhaa kutoka kwa wakaazi wa Khuzaa, Abasan na Bani Suheila wakitaka tukawaokoe na wakisema kuwa kuna watu wengi wameuawa na kujeruhiwa wakiwa chini ya vifusi vya nyumba zao," alisema mhudumu huyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.Picha: Reuters

Hata hivyo, gari mbili za kubebea wagonjwa na moja ya Shirika la Msalaba Mwekundu kwenye eneo hilo, zililazimika kurudi baada ya kushambuliwa kwa risasi, licha ya kuwa Msalaba Mwekundu wanasema walishawasiliana na jeshi la Israel hapo kabla.

Uwezekano wa usitishwaji mapigano

Kwengineko, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, amezungumza na wenzake wa Qatar na Uturuki juu ya kupatikana kwa usitishaji wa mapigano. Katika mazungumzo hayo, Kerry amesema anatazamia nchi hizo zitalishawishi kundi la Hamas kukubaliana na makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotayarishwa na Misri.

Afisa mmoja wa serikali ya Misri amesema kwamba inatazamiwa usitishaji wa muda wa mapigano kufikiwa kabla ya sikukuu ya Eid el Fitr inayotazamiwa wiki ijayo.

Hata hivyo, siasa zilizozunguka pande kadhaa zinazohusika na makubaliano hayo zinatajwa kuwa kikwazo kikuu cha makubaliano ya kudumu ya amani. Kwa upande mmoja, Marekani inaiunga mkono Israel kisiasa, kifedha na kijeshi, Misri ina uhasama na Hamas kwa kumuunga mkono kwake rais aliyepinduliwa na jeshi, Mohamed Mursi, Uturuki inaukosoa vikali utawala wa Misri na imeilaani hadharani sera ya Israel kuelekea Palestina, na Qatar imekuwa ikiiunga mkono Hamas licha ya kuwa pia rafiki wa Marekani.

Mkuu wa tawi la kisiasa la Hamas, Khalid Meshaal.
Mkuu wa tawi la kisiasa la Hamas, Khalid Meshaal.Picha: Getty Images/AFP

Kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Khalid Meshaal, alisema hapo jana kwamba hawatakubaliana na makubaliano yoyote ya amani yasiyokidhi masharti yao, likiwemo la kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Katikati ya siasa hizo, kufikia asubuhi ya leo tayari idadi ya Wapalestina waliokwishauawa imefikia 730, wengi wao wakiwa raia na robo yao wakiwa watoto, huku Israel ikipoteza wanajeshi 32 na raia watatu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo