Usitishaji mapigano Gaza wazingatiwa
6 Agosti 2014Mkuu wa ujasusi wa Misri amekutana Jumatano (06.08.2014) na ujumbe wa Wapalestina mjini Cairo ikiwa ni siku moja baada ya kukutana na wawakilishi wa Israel.Timu ya Wapalestina inaongozwa na afisa kutoka chama cha Fatah cha Rais Mahmoud Abbas kinachoungwa mkono na mataifa ya magharibi wakiwemo wajumbe kutoka Hamas na kundi la Islamic Jihad.
Afisa mmoja wa Misri amesema mazungumzo hayo ambayo sio ya moja kwa moja kati ya Wapalestina na Israel yanapiga hatua na ameweka wazi kwamba pande hizo hazikutani ana kwa ana na ameongeza kusema kwamba ni mapema mno kuzungumzia matokeo lakini wana matumaini.
Duru za Misri na Wapalestina zimesema wanatarajia kupata jibu la kwanza la Israel juu ya madai ya Wapalestina baadae leo hii.
Israel imeondowa vikosi vyake kutoka Ukanda wa Gaza hapo jana asubuhi na kuanza kuzingatia usitishaji wa mapigano wa saa 72 uliofikiwa chini ya usimamizi wa Misri katika mazungumzo na Hamas ikiwa kama ni hatua ya kwanza kufikia makubaliano yatakayodumu kwa muda mrefu.
Wapalestina wadai kukomeshwa kufungiwa kwa Gaza
Wapalestina wamekuwa wakitaka kukomeshwa kwa hatua ya Israel na Misri ya kuufungia Ukanda wa Gaza uliokumbwa na umaskini na kuachiliwa kwa wafungwa wakiwemo wale waliokamatwa katika msako wa mwezi wa Juni katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel baada ya vijana watatu wa Kiyahudi kutekwa nyara na kuuwawa.Israel imekuwa ikiyakataa madai hayo.
Msemaji wa waziri mkuu wa Israel Mark Regev amesema kwa Israel suala lililo muhimu kabisa ni suala la kuondolea silaha ukanda wa Gaza kwamba Hamas lazima ipokonywe silaha.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry katika mahojiano na kipindi cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC amezungumzia juu ya haja ya Hamas kusalimisha silaha zake za maroketi.
Wakaazi wa Gaza wazuru magofu ya nyumba zao
Huko Gaza ambao takriban watu nusu milioni wamepotezewa makaazi yao na umwagaji damu huo wa mwezi mmoja baadhi ya wakaazi wameondoka kwenye vituo vya Umoja wa Mataifa walikokuwa wamejihifadhi kwenda kuzuru vitongoji vyao ambapo takriban nyumba zote zimeangamizwa na mashambulizi ya mabomu ya Israel na harufu ya miili inayooza ilikuwa imehanikiza hewani.
Wakati huo huo ujumbe wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu ukiwemo ule kutoka Misri na Jordan utazuru Gaza hivi karibuni kuonyesha mshikamano wao na Wapalestina.
Ujumbe huo ambao utamjumuisha pia Mkuu wa Jumuiya ya Waarabu Nabi al Arabi pia utathmini mahitaji ya ujenzi mpya katika ukanda huo ulioathiriwa na vita.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga