Usitishaji wa mapigano Syria
4 Mei 2017Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema "Busara yetu ya pamoja ni kwamba kuanzishwa kwa kanda ya salama kutapelekea kuzidi kuituliza hali hiyo na kuimarisha usitishaji wa mapigano kuudhibiti mzozo huo wa umwagaji damu.Hili ni sharti muhimu kuwawezesha wahusika kuanza mazungumzo ambayo hatimae yanapaswa kurudisha heshima ya Syria kuitawala ardhi yake na kuiweka nchi hiyo chini ya uongozi ulioungana badala ya kudibitiwa na maoni yenye kudai yanawakilisha nguvu hii au ile ya kisiasa."
Wakikutana katika mji wa kitalii wa Sochi nchini Urusi hapo Jumatano (03.05.2017) Rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wameelezea matumaini yao kwamba serikali na waasi watakubali pendekezp la hivi karibuni kabisa kutoupalilia mzozo huo ambao hivi sasa uko katika mwaka wake wa sita na umegharimu maisha ya watu 400,000.
Uturuki na Urusi zimejizonga mno katika vita hivyo nchini Syria ambapo kila mmoja ina vikosi vyake ndani ya nchi hiyo wakati serikali ya Uturuki ikiunga mkono makundi mbali mbali ya upinzani nchini Syria huku Urusi ikiviunga mkono vikosi vya Rais Bashar al Assad.
Waasi wataka kusitishwa mashambulizi ya serikali
Kabla ya waasi kusitisha ushiriki wao katika mazungumzo yanayofanyika katika mji mkuu wa Kazakhstan Astana wawakilishi wa Urusi waliwasilisha kwa waasi pendekezo la kusitisha mapigano kwa maeneo manne nchini Syria ambapo pande zinazohasimiana zitatenganishwa na mipaka ya usalama.Mazungumzo hayo ya Astana ni mazungumzo rasmi ambapo wawakilishi wa serikali ya Syria na na waasi wamekuwa wakikutana kwa nyakati tafauti na maafisa wa serikali ya Urusi na wawakilishi wengine.
Waasi wa Syria kabla ya kuamuwa kurudi tena kwenye mazungumzo hayo leo hii ilisema hapo jana kwamba inasitisha ushiriki wao katika mazungumzo hayo ya amani na kudai kukomeshwa kwa mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na serikali katika maeneo yaliyoko chini ya udhibiti wao.
Akizungumza katika mkutano wa waandisdhi wa habari wa pamoja Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametahadharisha kwa kusema "Lazima tuchukuwe tahadhari kubwa sana wakati wa kutimiza wajibu wetu kama wadhamini,Kwa njia ya mazungumzo ya Astana tunajaribu kufikia lengo la kuimarisha usitishaji wa mapigano haraka iwezekanavyo lakini baadhi ya watu wanatumia wakati wao kujaribu kuhujumu mchakato huu. Mfano ulio dhahir kabisa na lile shambulio la silaha za sumu kwa mji wa Khan Sheikhoun."
Pendekezo lililowasilishwa kwa waasi mjini Astana linatenga maeneo manne nchini Syria ambapo mapigano yatasitishwa kati ya waasi na vikosi vya serikali.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP
Mhariri :Iddi Ssessanga