Usitishwaji mapigano Nagorno-Karabakh
5 Aprili 2016Wizara ya ulinzi ya Azerbaijan imesema operesheni za vikosi vya Azerbaijan na Karabakh zimesitishwa Jumanne (05.04.2016).
Senor Asratyan msemaji wa wizara ya ulinzi ya kujitangazia wenyewe ya eneo la Nagorno- Karabakh amethibitisha kwa shirika la habari la AP juu ya kufikiwa kwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.
Mwandishi wa AP katika eneo la mapambano la Azerbeijan amesikia milio ya mizinga mapema leo asubuhi lakini kulikuwa hakuna sauti za mapigano mapema wakati wa mchana.
Mapigano yalizuka mwishoni mwa juma kutoka kile kilichokuwa mzozo uliopowa.Kila upande umekuwa ukiushutumu mwingine kwa kuanzisha uchokozi huo na kwa kutumia silaha nzito.
Uhasama mbaya kabisa
Kuzuka huko kwa uhasama hakukuwahi kushuhudiwa tokea vita vilipomalizika hapo mwaka 1994 viliopelekea Nagorno- Karabakh ambayo rasmi ni miliki ya Azerbaijan kuwa chini ya vikosi vya kabila la Waarmenia katika eneo hilo na jeshi la Armenia.Vikosi vya Armenia pia vinakalia kwa mabavu maeneo kadhaa nje ya ardhi ya Karabakh.
Mzozo huo umechochewa na mvutano uliokuwa ukitokota kwa muda mrefu kati ya Waarmenia walio Wakristo na Waazeri walio Waislamu.Armenia juu ya kwamba inawaunga mkono wapiganaji wanaotaka kujitenga inasisitiza kwamba jeshi lake halihusiki katika mapigano hayo.
Mapema waziri wa serikali ya Azeri imesema wanajeshi 16 na raia mmoja wameuwawa siku mbili zilizopita katika mapigano wakati jeshi la Karabakh likiendelea kushambulia maeneo yake Jumatatu usiku.
Kufuatia tangazo hilo la kusitishwa kwa mapigano waziri wa mambo ya nje wa Azerbaijan Elmar Mamadyarov katika mazungumzo ya simu na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametowa wito wa kuwepo kwa machakato madhubuti wa kisiasa kutafuta ufumbuzi wa amani wa Karabakh.
Takwimu za maafa zatafautiana
Idadi ya maafa inayodaiwa na pande zote mbili imekuwa ikitafautiana sana tokea mapigano hayo yalipoanza hapo Jumamosi kwa Azerbaijan na Karabakh kurepoti kuuwawa kwa wanajeshi chungu nzima pengine hata mamia.
Gapanli kijiji kilioko kusini mwa Terter ndio kilioatharika zaidi na baadhi ya wanakijiji wamevikimbia vijiji vyao baada ya mapigano hayo ya mwishoni mwa juma.
Elmar Abdullayev amesema "tumewapeleka wake zetu, watoto wetu katika kijiji cha jirani lakini tutaendelea kubakia katika kijiji hiki hadi mwisho. Hii ni nchi yetu.Tutapigania haki zetu hadi mwisho."
Juhudi za kidiplomasia
Huko Armenia wizara ya ulinzi imeripoti mapigano kuenea kupindukia Karabakh kuelekea kaskazini - mashariki ya mpaka wa nchi hiyo ikisema maeneo yao yameshambuliwa na mizinga Jumatatu usiku na kumjeruhi mwanajeshi mmoja.
Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglo amesisitiza hapo Jumanne kuunga mkono kwa nchi yake mshirika wake wa jadi Azerbaijan kwa kusema itasimama pamoja na nchi hiyo hadi hapo ardhi yake inayokaliwa kwa mabavu itakapokombolewa.
Katika juhudi zilizokuwa zikitarajiwa sana waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ataelekea katika mji mkuu wa Azerbaijan hapo Alhamisi wakati waziri mkuu Dmitry Medvedev akitarajiwa kuwasili katika mji mkuu wa Armenia Yerevan siku hiyo hiyo.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP
Mhariri : Daniel Gakuba