1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti: Demokrasia yadhoofishwa kote ulimwenguni.

29 Aprili 2020

Wakfu wa masuala ya kidemokrasia ya nchini Ujerumani ya Bertelsman Stifttung, BTI umeonyesha kwamba kuna ongezeko la idadi ya watu wenye uongozi dhaifu na ambao hawazingatii kwa kiasi kikubwa misingi ya demokrasia.

https://p.dw.com/p/3bYDf
Hongkong | Protest | Journalist Fang Bin
Picha: Getty Images/AFP/I. Lawrence

Uchunguzi uliofanywa na wakfu wa masuala ya kidemokrasia ya nchini Ujerumani ya Bertelsman Stifttung, BTI umeonyesha kwamba kuna ongezeko la idadi ya watu wenye uongozi dhaifu na ambao hawazingatii kwa kiasi kikubwa misingi ya demokrasia. Uchunguzi huo umegundua kwamba kukosekana kwa usawa na ukandamizaji vinazidi kudidimiza uchumi wa kimataifa. 

Kulingana na ripoti ya karibuni iliyotolewa na wakfu huo wa BTI, uhuru wa kisiasa na utawala wa kisheria vimekuwa vikididimizwa miongoni mwa mataifa mengi kote ulimwenguni lakini pia tawala za kiimla zinazidi kuongeza ukandamizaji.

Wakfu huo wa Ujerumani umesema hapo jana kwamba sababu kubwa zinazochangia kuongezeka kwa ukandamizaji wa demokrasia kote ulimwenguni ni matumizi mabaya ya madaraka na teuzi zinazofanywa na wenye mamlaka, ambazo husababisha kuongeza ombwe ama kukosekana kwa usawa kijamii na hata kiuchumi.

Uchunguzi huo umesema, kushuka kwa wastani wa viwango vya demokrasia kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya tawala dhaifu na matumizi ya nguvu. Wakfu huo umeongeza kuwa athari za janga la hivi sasa la virusi vya corona linazidi kutishia demokrasia hata zaidi ulimwenguni kote.

Israel Tel Aviv Anti Netanjahu Demonstration Mundschutz
Waandamanaji nchini Israel, walioandamana kufuatia hali ya wasiwasi wa demokrasia nchini humo hivi karibuni.Picha: AFP/J. Guez

Viwango vya chini kabisa tangu kuanza kwa utafiti.

Tangu mwaka 2004, wakfu huo wa BTI ulikuwa ukifanya utafiti kuhusu hatua zinazopigwa katika nyanja za uchumi na siasa katika mataifa yanayoendelea kwa kila baada ya miaka miwili.

Kwa miaka sita mfululizo viwango vya BTI kuhusiana na hali ya demokrasia, uchumi na utawala vimeonyesha kushuka, na wakati huu vikiwa vimeshuka kwa kiwango cha chini kabisa tangu BTI ilipoanza uchunguzi wake. Miongoni mwa mataifa 137 ambayo yamefuatiliwa kwa kipindi hili, BTI inaona ni mataifa 74 tu yana demokrasia na mengine 63 yanakabiliwa na tawala za kibabe. 

Waandishi wa utafiti huo wamegundua kwamba kumekuwepo na uvurugwaji wa utawala wa sheria na uhuru wa umma katika mataifa ambayo awali yalikuwa yamesimamia vizuri demokrasia, wakiangazia kuongezeka kwa siasa kali za utaifa wa Kihindu nchini India, siasa za kizalendo nchini Brazil pamoja na utawala wenye mweleko wa kimabavu kwenye moja ya nchi mwanachama wa Ulaya, Hungary.

Sheria mpya yapiga marufuku kulala nje mitaani Hungary

Waandishi hao wamesema matukio kama hayo yanawakilisha kuongezeka kwa mgawanyiko ambao pia unadidimiza ushirikiano wa kimataifa na kuongeza kuwa hali hii huenda sambamba na ukandamizaji wa upinzani na watu wanaotoka kwenye jamii za walio wachache za kiimani ama makabila.

Utaifa na upendeleo sio masuala mapya, lakini yamekubalika kwa wakati huu ulimwenguni. Hata mataifa yaliyopigania sana demokrasia huko nyuma kama Poland na Hungary hivi sasa yanaonyesha wasiwasi mkubwa linapokuja suala la demokrasia na hali ya demokrasia, amesema Brigitte Mohn, mjumbe wa kamati tendaji ya wakfu huo wa BTI.

Mashirika: DW