1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utawala wa kijeshi waahidi kukabidhi madaraka

Oumilkher Hamidou1 Aprili 2012

Utawala wa kijeshi nchini Mali unaahidi kurejesha katiba ýa mwaka 1992 na taasisi za serikali ili kupata njia ya kufumbua mzozo nchini humo.

https://p.dw.com/p/14W6h
Mkutano mjini BbamakoPicha: Reuters

Kiongozi wa baraza la kijeshi linalotawala Mali ameahidi kuirudisha katiba ya nchi hiyo kuanzia Jumapili masaa machache kabla ya muda wa mwisho uliowekwa

na mataifa jirani ya Afrika magharibi kuanza kukabidhi madaraka,wakati waasi wakiuzingira mji wa kale wa kibiashara wa Timbuktu.

Kapteni Amadou Sanogo ambaye aliongoza mapinduzi ya kijeshi tarehe 22 mwezi wa Machi pia ameahidi kuzirudisha tena madarakani taasisi zote za serikali kabla ya kurudisha madaraka kwa wananchi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia.

Ametowa ahadi hiyo baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika magharibi ya nchi wanachama 15 kutaka kuanza kukabidhi madaraka usiku wa manane Jumapili ya tarehe 01.04.2012 venginevyo atakabiliwa na vikwazo ikiwemo kufungwa kwa mipaka inayoizunguka nchi hiyo isiokuwa na bahari.

Lengo la mapinduzi hayo yaliofanywa na wanajeshi wenye manun'guniko ni kuimarisha mapambano dhidi ya waasi wa kaskazini.Lakini mapinduzi hayo yamekwenda kombo kwa kushajiisha uasi wa Tuareg kuteka miji mipya katika harakati za kuwa na taifa lao kaskazini mwa Mali.

Amadou Sanogo
Amadou SanogoPicha: Reuters

Repoti nyengine zinasema tayari wameuteka mji wa Timbuktu na kwamba watatangaza rasmi taifa lao huru linaloitwa AZAWAD.

Sanogo amesema katika taarifa iliosomwa katika kambi ya kijeshi nje ya mji mkuu wa Bamako kwamba wanaahidi kwa dhati kuirudisha katiba ya Mali ya tarehe Pili Februari mwaka 1992 kuanzia sasa pamoja na taasisi za Jamhuri hiyo.

Sanogo kapteni asiyejulikana sana aliepatiwa mafunzo nchini Marekani amesema baraza la kijeshi limekubali kushauriana na vyama vya kisiasa kuunda chombo cha mpito kwa lengo la kuanzisha uchaguzi wa amani,huru,wa uwazi na wa demokrasia ambao wanajeshi hao hawatoshiriki.

Jumuiya ya ECOWAS haikutowa jibu mara moja kuhusiana na uamuzi huo uliotangazwa na Sanogo.Hata hivyo kurudishwa tena kwa katiba na taasisi za taifa yalikuwa ni mambo mawili yaliotajwa hapo awali na mjumbe wa Burkina Faso Rais Balise Compaore ambaye ni msuluhishi wa mzozo huo wa Mali kuwa ni masharti muhimu kwa Mali kuepuka kuwekewa vikwazo.

Waziri wa mambo ya nje wa Burkina Faso Djibril Bassolet ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwa njia ya simu muda mfupi kabla ya kutolewa kwa taarifa hiyo ya Sanogo kwamba "Tunataka kuwa waangalifu,inabidi twende hatua kwa hatua" akionya juu ya hatari ya kuwepo kwa ombwe la madaraka.

Waasi watwaa miji kaskazini

Mji wenye makao makuu ya serikali wa Kidal umetekwa hapo Ijumaa na kufuatiwa kutekwa kwa mji wenye kambi ya kijeshi wa Gao hapo Jumamosi.Kutekwa kwa mji wa Timbuktu kwa kiasi kikubwa kutakuwa kumekamilisha mpango wa waasi wa Tuareg kulinyakua eneo la kaskazini mwa Mali ambao ni eneo la jangwani kubwa kuliko hata nchi nzima ya Ufaransa.

Chama cha Vuguvugu la Taifa la Ukombozi wa Azawad (MNLA) kimetangaza kwamba jeshi lake linautwaa mji wa Timbuktu kun'gowa mabaki ya mamlaka ya kisiasa na kijeshi ya Mali.

Flüchtlinge aus Mali in Flüchtlingslager in Niger
WakimbiziPicha: Fatoumata Diabate

Mapema wakaazi wa mji huo wameripoti kwamba vikosi vya kijeshi vilikuwa vikiutelekeza mji huo na kuwacha ulinzi wake kwa wanamgambo wenyeji ambao waliingia mitaani na kufyatuwa risasi hewani.

Inaelezwa kambi ya kijeshi iko tupu na takriban wanajeshi wote kutoka kusini mwa Mali wamekimbia na kuwaachilia Waarabu wenye asili ya Mali tu wauhami mji huo.

Timbuktu kwa karne nyingi ulikuwa ni kituo cha biashara katika Sahara na ukijulikana kwa dhahabu yake, watumwa na bidhaa nyengine lakini hadhi ya mji huo ilikuja kushuka kabla ya hata kuja kukaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika karne ya 19.

Majribio ya kuendeleta utalii katika mji huo yamekwamishwa kutokana na kuongezeka kwa ukosefu wa usalama ikiwa ni pamoja na kutekwa nyara kwa raia wa mataifa ya magharibi kunakofanywa na mawakala wa kundi la Al Qaeda.

Mwandishi:Mohamed Dahman/RTRE

Mhariri:Hamidou Oummilkheir