Utulivu warejea nchini Ufaransa baada ya machafuko
3 Julai 2023Hali ya utulivu imeanza kurejea nchini Ufaransa huku mameya nchini humo wakitowa mwito wa kufanyika mikutano ya kupinga maandamano ya vurugu yaliyoitikisa nchi kwa kiasi cha wiki moja kufuatia mauaji yaliyofanywa na polisi dhidi ya mvulana mwenye umri wa miaka 17 mwenye asili ya Kiarabu.
Kwa mara nyingine, wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa imechukua hatua ya kupeleka polisi na askari 45,000 wa kikosi maalum kote nchini humo usiku wa kuamkia leo Jumatatu, kama ambavyo wizara hiyo ilichukua hatua kama hiyo siku mbili zilizopita kujaribu kuzima machafuko.
Soma pia: Ghasia zimepungua Ufaransa
Rais Emmanuel Macron jana Jumapili aliitisha mkutano wa dharura na baraza lake la mawaziri, huku ikiarifiwa kwamba hiyo hiyo jana waandamanaji waliyalenga makaazi ya meya mmoja nje ya Paris kwa kuvurumisha gari lililotiwa moto na kumjeruhi mkewe. Tukio hilo limelaaniwa nchi nzima.
Aidha mfanyakazi mmoja wa zima moto mwenye umri wa miaka 24 alipoteza maisha akipambana kuzima moto katika eneo la kuegesha magari kwenye mji wa Seine-Saint-Denis kaskazini mwa Paris.
Taarifa ya chama cha mameya nchini humo imesema kwamba katika maeneo mengi ya Ufaransa kumetokea machafuko makubwa yaliyolenga majengo na alama za Jamhuri.
Serikali imesema inapambana kuzima vurugu hizo pamoja uporaji katika maeneo mbali mbali ya nchi uliochochewa na tukio la kuuwawa na polisi wa Trafiki, kwa kupigwa risasi kijana Nahel mwenye umri wa miaka 17 baada ya kushindwa kusimamisha gari alipotakiwa kusimama mnamo siku ya Jumanne wiki iliyopita.
Tukio la kuuwawa kijana huyo limeibua hasira na tuhuma za wananchi kuhusu jeshi la polisi kuendeleza vitendo vya ubaguzi wa rangi nchini Ufaransa.
Hivi sasa inaelezwa kwamba kuna hali ya utulivu kiasi japo wizara ya mambo ya ndani imesema usiku wa kuamkia leo watu 157 walikamatwa kufuatia vurugu za nchi nzima na baadhi yao walipelekwa rumande tangu Jumamosi, huku maafisa watatu wakijeruhiwa.
Soma pia: Polisi nchini Ufaransa yawakamata zaidi ya watu 719 wakati wa ghasia za kupinga ukatili wa polisi
Wengi wa wakaazi wameshusha pumzi kufuatia kurudi kwa hali ya utulivu japo yapo pia masikitiko kutokana na uharibifu uliofanyika nchi nzima. Josie Oranger mwenye umri wa miaka 49 ni mkaazi wa Nanterre.
"Nimefurahi sana utulivu unarejea. Na wakati huo huo sina furaha kutokana na tulichokipitia. Kwa sababu kuna watu hatujui walifanya nini kupata magari yao, maduka, biashara zao. Pengine wako waliochukua mkopo kupata walivyokuwa navyo. Halafu ndani ya usiku mmoja wanapoteza kila kitu kutokana na machafuko. Sio makosa yao kwa kila kilichotokea.''
Jana, bibi yake kijana Nahel aliyeuwawa, alitowa mwito wa utulivu akisema waandamanaji wanaofanya vurugu walikuwa wakitumia fursa ya kijana huyo kufanya hujuma zao.
Machafuko ya Ufaransa yameonesha mgogoro mpya unaomkabili Rais Macron baada ya nchi hiyo kuandamwa na maandamano kwa miezi baada ya kuongezwa umri wa kustaafu.
Rais huyo aliyeakhirisha ziara yake ya kiserikali nchini Ujerumani iliyokuwa imepangwa kuanza jana Jumapili, leo atakutana na viongozi wa mabaraza mawili ya bunge pamoja na mameya wa miji 220 iliyokumbwa na machafuko.