Utulivu warejea Gaza baada ya siku mbili za machafuko
10 Agosti 2018Makubaliano hayo ya kusitisha mapigano huenda yakakabiliwa na changamoto kubwa kufuatia wapalestina mjini Gaza kuamua kuanza tena maandamano yao ya kila wiki, ambayo mara kwa mara yanakumbwa na vurugu.
Baada ya usiku mtulivu, jeshi la Israel liliwaambia wakaazi wake katika eneo la kusini waliokuwa katika maeneo ya kujikinga dhidi ya makombora kwamba kwa sasa wanaweza kurejea katika hali zao za kawaida.
Ongezeko la makombora yaliyovurumishwa mpakani mwa Israel na Gaza pamoja na mashambulizi ya angani katika wiki za hivi karibuni yamesababisha Umoja wa Mataifa na Misri kujaribu kufikia makubaliano kati ya pande hizo mbili hasimu ili kuzuwia mgogoro mkubwa zaidi.
Katika vurugu za siku mbili zilizopita mwanamke mmoja wa kipalestina aliyekuwa mja mzito, mwanawe wa miaka 18 pamoja na mwanamgambo mmoja wa Hamas waliuwawa huku watu takriban 7 wakijeruhiwa kutokana na maroketi yaliorushwa nchini Israel.
Hata hivyo maafisa wa Palestina wanasema makubaliano yamefikiwa kupitia mpatanishi ambaye ni Misri, lakini bado hapajakuwa na tamko rasmi kutoka upande wa Israel la kukubali kufikia makubaliano ya aina yoyote na kundi la Hamas. Kundi hilo la wanamgambo la Hamas linalotambuliwa na mataifa mengi ya Magharibi kama shirika la kigaidi tayari limepigana vita mara tatu na Israel ndani ya muongo mmoja uliopita.
Kundi la Hamas lasema kwa utulivu kamili ni lazima Israel ijirekebishe
Kabla ya makubaliano hayo kufikiwa hapo jana msemaji wa Hamas Fawzi Barhoum alisema siku za usoni za Palestina pamoja na kufanikiwa kwa kundi lolote la upatanishi ni lazima Israel ijirekebishe. Israel kwa upande wake kupitia msemaji wa jeshi Luteni kanali Jonathan Conricus imesema itaendelea kuilinda Israel pamoja na watu wake na iko tayari kukabiliana na hali yoyote ile.
Lakini huku utulivu ukiwa bado unashuhudiwa mpakani mwa Israel na Gaza, waandaaji wa maandamano ya mpakani dhidi ya Israel wameonekana wakipita kwa gari katika maeneo ya Gaza wakiwaita watu kupitia vipaza sauti kujitokeza kwa wingi katika maandamano yaliopangiwa kufanyika hii leo.
Raia wa Gaza wamekuwa wakiandamana kila wiki kuanzia tarehe 30 mwezi Machi wakitaka haki yao ya kurejea nyumbani. Katika maandamano hayo jeshi la Israel limesababisha mauaji ya wapalestina 158 huku mlenga shabaha wa Palestina akisababisha kifo cha mwanajeshi mmoja wa Israel.
Mwandishi Amina Abubakar/AFP/dpa/Reuters
Mhariri: Josephat Charo