1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki kuimarisha uhusiano wake na Umoja wa Ulaya

19 Januari 2021

Mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na Uturuki wameashiria mwanzo mpya katika uhusiano baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya ulioshuhudia mivutano huko nyuma.

https://p.dw.com/p/3o6wk
Türkei Heiko Maas und Mevlut Cavusoglu
Picha: Cem Ozdel/AA/picture alliance

Uturuki imekubali kukaa kwenye meza ya mazungumzo na jirani yake Ugiriki tarehe 25 mwezi huu wa Januari nchi zote hizo mbili ni wanachama wa jumuiya ya kujihami ya Nato. Na kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2016 huu ndio mkutano wa mwanzo utakaolenga kutatua baadhi ya tafauti zao kuhusiana na suala la mipaka ya bahari na utafiti wa uchimbaji wa nishati ya gesi kwenye eneo la mashariki mwa bahari ya Meditterania.

Hatua hii imemridhisha waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas aliyekwenda Uturuki kukutana na mwenzake Mevlut Cavusoglu. Heiko Maasamesema kuanza tena kwa mazungumzo hayo ya mashauriano ni dalili nzuri kwa ajili ya uthabiti wa eneo zima.

''Kilichobakia hivi sasa ni kuyamaliza katika kipindi cha mwanzo wa mwaka huu yale mazungumzo magumu ya mwaka jana. Tunalipokea tangazo kwamba nyinyi Uturuki mnataka kuanza tena mazungumzo kuhusu eneo la bahari la Mashariki mwa meditterania wiki ijayo.Ninachoweza kusema ni kwamba sizungumzi kwa niaba ya serikali ya Ujerumani tu bali kwa niaba ya Umoja wa Ulaya,hii ni hatua ya kwanza kuelekea suluhisho la kidiplomasia katika mzozo huu na ishara nzuri kwa uthabiti wa kanda nzima''

Türkisches Forschungsschiff Oruc Reis zur Gaserkundung im Mittelmeer
Meli ya utafiti ya Uturuki katika eneo la bhari linalozozaniwaPicha: picture-alliance/AP/DHA/I. Laleli

Uturuki na Ugiriki ni nchi ambazo kwa muda mrefu zinavutana kuhusu raslimali ya hifadhi ya gesi pamoja na mipaka ya bahari huku kila mmoja akidai kuwa mwenye haki ya kutafiti na kuchimba nishati hiyo ya gesi katika eneo la Mashariki mwa bahari ya Meditterania.

Na mwaka jana Ugiriki na Cyprus ziliishuhudia Uturuki ikitunisha misuli kwa kupeleka meli yake ya utafiti katika eneo hilo la bahari linalozozaniwa, na washirika wao katika Umoja wa Ulaya nao wakapeleka meli zao katika eneo hilo kuiunga mkono Ugiriki katika madai yake ambapo ilishuhudiwa Uturuki na Ugiriki zikionesha nguvu za kijeshi kwa kutumia meli na ndege za kivita.

Infografik Karte Grenze zwischen Griechenland und der Türkei EN
Ugiriki na jirani yake Uturuki

Hapa ndipo Umoja wa Ulaya ukatishia kuichukulia hatua kali Uturuki mwezi Desemba kufuatia shughuli zake hizo za kufanya utafiti katika eneo hilo la bahari. Suala hili sasa litathminiwa tena katika mkutano wa kilele wa Umoja huo mwezi Marchi.

Lakini pia Cavusoglu,waziri wa mambo ya nje wa Uturuki amesema kwamba mazungumzo na Umoja wa Ulaya,na Ugiriki yaliyoanzishwa na nchi yake hayahusiani kwa namna yoyote na vikwazo vya Umoja huo huku akisisitiza kwamba wala serikali ya mjini Ankara haiogopi hatua za vikwazo. Juu ya hilo Cavusoglu anasema Uturuki iko tayari kwa mazungumzo bila ya masharti yoyote tafauti na Ugiriki.

Ameionyooshea kidole nchi hiyo akisema inaendelea na vitendo vyake vya uchokozi mpaka hivi sasa. Kwa upande mwingine Heiko Maas amezishawishi pande zote kuangalia suluhisho la kudumu mapema iwezekanavyo akisema Uturuki na Ugiriki zina nafasi nzuri ya kuumaliza mvutano wao wa Mashariki mwa bahari ya Meditterania.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW