1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Mageuzi ya katiba Cuba Magazetini

Oumilkheir Hamidou
14 Agosti 2018

Mgogoro wa kiuchumi nchini Uturuki na madhara yake kwa nchi za Ulaya , mjadala kuhusu mageuzi ya katiba Cuba na mjadala kama CDU wasivinyemelee vyama vya mrengo wa kushoto ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/3380o
Türkei, Wahlen
Picha: picture-alliance/E.Gurel

Tunaanzia Uturuki ambako kila mwanablogu, mwandishi habari na wengineo, wanaoeneza habari za kutisha kuhusu hali ya kiuchumi, wanaandamwa. Chanzo ni kuporomoka vibaya sana sarafu ya nchi hiyo Lira kufuatia vikwazo vya Marekani. Madhara ya mzozo wa kiuchumi nchini Uturuki yataziathiri nchi nyingi za dunia ikiwa ni pamoja na Ujerumani. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika:

"Katika wakati wa misukosuko, majadiliano ni muhimu. Na hali hiyo inahusu pia kuendelezwa mawasiliano na Recep Tayyip Erdogan. Haimaanishi kwamba rais huyo wa Uturuki anabembelezwa. Hasha, lakini uchumi wa Uturuki ukiporomoka, kwa sababu ya mvutano usioeleweka pamoja na rais wa Marekani, basi hali hiyo haitakuwa kwa masilahi ya Ujerumani wala kwa watu wanaoishi Uturuki. Kwa hivyo Merkel atabidi ajaribu kupatanisha. Bora hivyo kuliko mengine."

Erdogan anaamini atashinda kama alivyoishinda Njama ya Mapinduzi 2016

"Mannheimer Morgen" linauchambua mgogoro wa kiuchumi wa Uturuki na kuashiria Erdogan ndiye atakayeibuka na ushindi. Gazeti linaendelea kuandika:

"Mgogoro wa sarafu ya Uturuki bado haujamuathiri rais Recep Tayyip Erdogan. Kinyume kabisa, anaonekana kana kwamba yeye ndiye atakayeibuka na ushindi. Erdogan anamtaja rais Donald Trump kuwa chanzo cha "vita vya kiuchumi" vinavyotangazwa na Marekani dhidi ya Uturuki. Rais wa Uturuki analinganisha hali hii na ile ya njama iliyoshindwa ya mapinduzi mwaka 2016. Kama ilivyokuwa wakati ule, anaamini na safari hii pia atamudu kishindo na kujiimarisha madarakani. Na wafuasi wake bado wanamuamini."

Cuba yajiandaa kwa Mageuzi ya Katiba

Mjadala umepamba moto nchini Cuba kuhusu suala la kufanyiwa marekebisho katiba ya kisiwa hicho ambacho hadi sasa kimekuwa kikifuata siasa ya kikoministi. Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linaandika:

"Dalili ya kwanza ya Cuba kuujongelea ubepari ameionyesha mwenyewe Fidel Castro. Alipovua sare yake ya kijeshi, mfuasi huyo wa nadharia ya Marx alikuwa kila wakati akionekana na mavazi ya spoti- kanda tatu-Adidas kutoka mkoa wa kusini mwa Ujerumani. Miaka miwili baada ya kifo cha Fidel Castro mjadala umehanikiza kote nchini Cuba kama katiba ifanyiwe marekebisho nchini humo. Vyovyote vile itakavyokuwa mfumo wa vyama vingi sawa na uchaguzi huru na wa siri itasalia kuwa ndoto kwa wacuba wengi.

Mtaka cha mvunguni huinama

Chaguzi tatu za majimbo zitaitishwa nchini Ujerumani mwakani. Kinyang'anyiro cha kuania kura kimeshaanza. Katika wakati ambapo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani" AfD kinazidi kuwavutia wapiga kura, mjadala umezuka ndani ya chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU, kama haitokuwa bora pia kujongelea vyama vya mrengo wa kushoto, mbali na chama cha Social Democratic, SPD. Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linaandika:

Ili kuunda serikali ya muungano pamoja na vyama vya mrengo wa kushoto, wana CDU watalazimika kwanza kuwa na mipango inayojongelea zaidi na ile ya vyama hivyo kuliko vile ilivyokuwa hadi sasa pamoja na SPD. Na hilo wana CDU hawatolitaka, kwa sababu sio tu wana Christian Democratic watawapoteza wapiga kura wao bali pia watawafanya wafuasi wao waelemee upande wa chama cha AfD.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo