1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yawarejesha makwao wapiganaji wa kigeni wa IS.

12 Novemba 2019

Uturuki imeanza kuwarejesha wapiganaji wa kigeni wa kundi linalojiita dola la kiislamu IS kwenye mataifa yao, zikiwemo Ujerumani, Denmark na Marekani katika mpango wa kuwarejesha makwao wafungwa wa kundi hilo,

https://p.dw.com/p/3SrZX
Türkei Verhaftung mutmaßlicher IS-Kämpfer
Picha: Getty Images/AFPB. Kilic

Uturuki inasema kuwa imewakamata wanamgambo 287 katika eneo la kaskazini mwa Syria na tayari inawazuia mamia ya washukiwa wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS. Taifa hilo limeyashtumu mataifa ya Ulaya kwa kuchelewa kuwachukuwa raia wake waliokwenda kupigana nchini Syria.

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Suleyman Soylu, alisema kuwa nchi yake ingelianza kuwarejesha wapiganaji wa kigeni wa kundi hilo la IS katika mataifa yao kuanzia jana Jumatatu hata kama mataifa wanapotoka wapiganaji hao yameshawafutia uraia wao. Msemaji wa wizara hiyo, Ismail Catakii, amesema kuwa tayari raia mmoja wa Marekani na Ujerumani walisharejeshwa makwao hapo jana. Hata hivyo, hakutaja walipopelekwa ijapokuwa Uturuki imerejelea kusema kuwa wafungwa hao watarejeshwa katika mataifa yao asilia.

Watu wengine 23 watakaorejeshwa makwao katika siku chache zijazo wote ni kutoka mataifa ya Ulaya ikiwa ni pamoja na raia mmoja wa Denmark, wawili wa Ireland, tisa wa Ujerumani na 11 kutoka Ufaransa. Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema kuwa Uturuki imeifahamisha kuhusu watu 10 - watatu wanaume, watano wanawake na watoto wawili. Msemaji wa wizara hiyo amesema kuwa hafahamu iwapo watu hao ni wapiganaji wa kundi hilo la wanamgambo la IS, lakini wizara haikupinga kuhusu uraia wao. Wizara hiyo imesema kuwa watu saba wanatarajiwa siku ya Alhamisi na wawili siku ya Ijumaa.

Süleyman Soylu
Waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki Suleyman SoyluPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Ozbilici

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Horst Seehofer, amewahakikishia raia wa Ujeruamni kuwa kila kisa kitachunguzwa kikamilifu na maafisa wa serikali ya Ujerumani na kwamba watafanya kila wawezalo kuwazuia watu hao watakaorejeshwa kwa kuwa na ushirikiano na kundi la IS wasiwe tishio nchini Ujerumani. Huku serikali ya Ujerumani na Denmark zikithibtisha kuwa zilifahamu kuhusu mipango ya Uturuki, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly, amesema kuwa hakufahamu kuhusu hatua hiyo.

Marekani haikujibu mara moja kuhusu tangazo hilo Uturuki. Gazeti la Sabah nchini Uturuki lililo na ukaribu na serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan limeripoti kuwa raia wa Marekani aliyerejeshwa nchini mwake amekwama katika eneo lisilo na umiliki lililo na ulinzi mkali wa kijeshi kati ya mipaka ya Ugiriki na Uturuki.

Nchini Denmark, Waziri wa Sheria Nick Hakkerup aliliambia shirika la habari la TV2 kuwa raia yeyote wa nchi hiyo aliyepigania kundi hilo la wanamgambo la IS na kurejeshwa nchini humo ''anapaswa kupata adhabu kali''.  Tayari mahakama moja ya Denmark ilishaamua kuwa nchi hiyo inapaswa kuwarejesha nchini humo watoto ambao mama zao walikwenda Syria kujiunga na makundi ya itikadi kali.Nchini Bosnia, serikali ilitangaza jana kuwa raia wake waliopigana katika kundi hilo la IS wanaweza kurejea nchini humo.