Rais Erdogan asema mapigano hayatakoma
30 Agosti 2016Shirika hilo la habari la Dogan limesema zaidi ya makombora 108 yalivurumishwa katika maeneo 21 ya wapiganaji wa kikurdi. Hata hivyo Marekani inazidi kuwa na wasiwasi kwamba mshirika wao katika Jumuiya ya Kujihami NATO, Uturuki na wapiganaji wa kikurdi nchini Syria waliyoandaliwa na Marekani chini ya wanamgambo wa kikurdi wa kundi la SDF wameingia katika mgogoro Kaskazini mwa Syria baada ya jeshi la Uturuki kuingia huko wiki iliyopita.
"Tumezitolea mwito pande zote mbili ziache kupigana wenyewe kwa wenyewe na kuendelea kuunganisha nguvu zao kupigana na kundi la wanamgambo wa dola la kiislamu, hilo ndilo lililotufanya tushirikiane na makundi yote mawili," alisema Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter.
Carter ameongeza kwamba tayari wameshaiomba Uturuki kuelekeza mashambulizi yake dhidi ya IS na siyo kupigana na vikosi vya ulinzi vya Syria.
Ashton Carter pamoja na Naibu mshauri wa usalama wa taifa katika ikulu ya Marekani Ben Rhodes, kwa pamoja wamesema vikosi vya kikurdi nchini Syria vinapaswa kujiondoa Mashariki mwa mto Euphrates.
Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan, asema operesheni yao bado inaendelea
Hata hivyo rais wa Syria Tayyip Erdogan amesema operesheni yao inafanyika kwa ushirikiano wa muungano wa Kimataifa unaoongozwa na Marekani na kuapa kwamba mashambulio Kaskazini mwa Syria yataendelea, hadi kitisho kutoka kwa wanamgambo wa IS na wapiganaji wa kikurdi kitakapomalizika.
Uturuki inawasiwasi juu ya wakurdi wa Syria kuwa na mfungamano na waasi wa kikurdi wanaopigana katika ardhi yake. Wakurdi ni wachache katika nchi hizo mbili Uturuki na Syria na wamekuwa wakilalama juu ya kubaguliwa. Lakini afisa wa Marekani ameweka wazi kwamba wanaunga mkono hatua za Uturuki kuwaondoa wanamgambo wa IS katika eneo la mpakani mwa Syria na Uturuki.
Wakati huo huo msemaji wa kundi la wakurdi Kaskazini mwa Syria Shervan Darwish amedai kikosi cha Uturuki kina lengo la kuwaangamiza watu wa maeneo hayo.
"Lengo la Uturuki ni kuwaangamiza watu wa eneo hili na kuwaweka waislamu wenye itikadi kali” alisema Darwish. Ameongeza kuwa mashambulio ya angani yanayofanywa na Uturuki yamesababisha mauaji ya raia wengi madai ambayo afisa mmoja wa Uturuki ameyakanusha vikali wiki hii. Darwisha Aidha ametaka uchunguzi wa kimataifa kufanywa juu ya mashambulio yanayofanywa na Uturuki.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/ Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga