Uturuki yaendeleza mashambulizi Syria
12 Oktoba 2019Hayo yanaendelea huku kukiwa na dalili ndogo ya kusimamishwa kwa mashambulizi hayo licha ya ukosoaji unaotolewa kimataifa. Mashambulizi hayo ya Uturuki yamesogea hadi katikati mwa mji wa Ras-Al Ayn, ambao ni mji muhimu kaskazini mashariki mwa Syria.
Shirika la habari la serikali ya Uturuki Anadolu, limesema vikosi pinzani vya Syria vinavyoshirikiana na Uturuki, vimeidhibiti barabara ya M-4 inayounganisha miji ya Manbij and Qamishli. Vikosi vya Uturuki pia vimeidhibiti njia nyingine inayounganisha mji wa Kaskazini Mashariki mwa Hassakeh na Aleppo ambao ni mji mkubwa zaidi wa Syria na kituo cha biashara, kulingana na shirika la kufuatilia haki za binadamu la Syria. Idadi ya waliouawa kutokana na mashambulizi ya Uturuki kaskazini mashariki mwa Syria imefikia watu 30. limeongeza shirika hilo.
Uturuki, imechukua hatua ya kuingiza vikosi vyake ndani zaidi Kaskazini mwa Syria baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuacha wazi njia kwa vikosi vya anga na ardhini vya Uturuki kwa kuwaondoa wanajeshi wake kwenye eneo hilo na kusema kuwa hataki kuendelea kujihusisha na vita visivyokwisha.
Uamuzi wa Trump haukuungwa mkono na vyama vya siasa
Uamuzi huo wa Trump ulikosolewa na chama chake cha Republican pamoja na chama cha Democratic kwa madai kuwa anahatarisha usalama wa eneo hilo na kuyaweka hatarini maisha ya Wakurdi ambao ni washirika wa Syria walioliangusha kundi linalojiita dola la Kiislamu.
Wapiganaji wa Kikurdi wakiongozwa na vikosi vya Syria walikuwa washirika wakuu wa Marekani katika vita dhidi ya dola la Kiislamu ambalo lilipoteza wapiganaji 11,000 katika vita vilivyodumu kwa karibu miaka mitano.
Tangu Jumatano, wanajeshi wa Uturuki na wapiganaji wa Syria wanaoungwa mkono na Uturuki wamekuwa wakiendeleza mashambulizi ya anga hadi katika barabara ya Manbij-Qamishli, kilometa 30 kusini mwa mpaka wa Uturuki.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa takribani watu 100,000 wameyahama makazi yao tangu Jumatano iliyopita na kwamba masoko, shule na hospitali pia zimefungwa. Mashirika ya kutoa misaada yameonya juu ya uwezekano wa kutokea mgogoro wa kiutu huku takribani watu nusu milioni wakiwa hatarini Kaskazini mashariki mwa Syria.
Ijumaa iliyopita Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema, Uturuki haitoacha mashambulizi hadi vikosi vya Kikurdi vya Syria vitakapoondoka na kurudi nyuma ya mpaka kwa kilometa 32. Vikosi vya Uturuki, vinalenga kuwaondoa wapiganaji wa Kikurdi katika miji iliyo kwenye eneo la mpaka la Syria vikisema uwepo wa wapiganaji hao ni tishio kwa usalama wa Taifa.
Kutokana na mashambulizi yanayoendelea, Rais wa Ufaransa alimwonya Rais Wa Marekani Donald Trump kuwa hatua za kijeshi za Uturuki zinaweza kusababisha kuibuka tena kwa shughuli za kundi la dola la Kiislamu. Macron, alitoa wito wa kuitaka uturuki isimamishe mashambulizi mara moja.
ap,afp,rtre