1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki yaidhinisha sheria ya mitandao yenye nguvu mpya

29 Julai 2020

Bunge la Uturuki siku ya Jumatano liliidhinisha sheria itakayoipa serikali ya nchi hiyo nguvu zaidi za kudhibiti mitandao ya kijamii licha ya wasiwasi unaoongezeka kuhusu udhibiti huo.

https://p.dw.com/p/3g8KF
Türkei Parlament Ankara
Picha: Getty Images/AFP/A. Altan

Sheria hiyo inahitaji kampuni za mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Twitter kuwa na ofisi za uwakilishi nchini Uturuki kushughulikia malalamishi dhidi ya habari katika mitandao yao. Serikali inasema kuwa sheria hiyo ilihitajika kukabiliana na uhalifu wa mitandaoni na kuwalinda watumiaji.

Akizungumza bungeni Jumatano asubuhi, mbunge wa chama tawala Rumeysa Kadak, alisema kuwa sheria hiyo itatumika kuondoa taarifa zinazohusika na unyanyasaji wa mtandaoni na uchokozi dhidi ya wanawake.

Lakini wabunge wa upinzani wanasema kuwa sheria hiyo itakandamiza uhuru wa kujieleza katika nchi hiyo ambayo tayari vyombo vya habari viko chini ya udhibiti mkali wa serikali na mamia ya wanahabari kufungwa. Wabunge hao waliita sharia hiyo '' sheria ya udhibiti.''

Türkei Ankara Parlament Coronavirus
Wabunge wa bunge la Uturuki wakiunga mkono hoja.Picha: DHA

Hatua zitakazochukuliwa dhidi ya kampuni zitakazokaidi ya serikali

Iwapo kampuni za mitandao ya kijamii zitakataa kuweka waakilishi nchini humo, sheria hiyo inaruhusu kutoza faini, kupiga marufuku matangazo na kupunguza kiasi cha data kinachoweza kusambazwa kutoka eneo moja hadi lingine mtandaoni katika muda wa kiasi fulani.Hatua hiyo itamaanisha kuwa mitandao ya kijamii itakuwa na kasi ya chini ya matumizi.

Mwakilishi huyo atakuwa na jukumu la kujibu maombi ya kibinafsi ya kuondoa taarifa zinazokiuka usiri wa mtu na haki za kibinafsi katika muda wa saa 48 ama kutoa sababu za kukataa kuchukuwa hatua hiyo.

Kampuni hiyo itawajibikia hasara itayosababishwa na kutoondolewa kwa taarifa hizo ama kufungiwa katika muda wa saa 24.

Ombi la kutatiza kutoka kwa serikali

Kile kinachoshtua zaidi ni kwamba sheria hiyo ya kurasa tisa pia itazitaka kampuni hizo za mitandao ya kijamii kuhifadhi maelezo ya watumiaji wa mitandao hiyo nchini humo.

Türkei l Youtube-Sperre
Sheria mpya itaipa nguvu serikali kudhibiti zaidi mitandao ya mawasiliano ya internet.Picha: Imago/R. Peters

Mamia ya watu wamechunguzwa na wengine kukamatwa kutokana na kuweka taarifa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na janga la virusi vya corona , upinzani kuhusu mashambulizi ya jeshi la nchi hiyo ng'ambo ama kumtusi rais Recep Tayyip Erdogan na maafisa wengine wa serikali.

Erdogan ametaka kutungwa kwa sheria hiyo na kuapa ‘'kudhibiti mitandao ya kijamii'' na kuondoa ukosefu wa nidhamu.

Yaman Akdeniz, mwanaharakati wa mitandao ya kijamii ambaye pia ni msomi, alituma ujumbe katika mtandao wa twitter akisema kuwa kipindi cha giza kinaanza tena nchini Uturuki kwa sheria hiyo mpya.

Soma pia Msikiti wa Hagia Sophia wafunguliwa rasmi Istanbul

Alisema kuwa sheria hiyo itatumika kuondoa taarifa muhimu kwa serikali mbali na kuwalinda watumiaji.

Hapo jana Jumanne, makundi za kutetea haki na shirika la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa yalipinga muswada huo kabla ya kura kupigwa huku shirika la Amnesty Imternational likiitaja kuwa ‘' ya kidikteta.''

Athari za sheria hiyo

Mtafiti wa shirika la Amnesty International nchini UturukiAndrew Gardner, alisema iwapo muswada huo utapitishwa, utaongeza kwa kiasi kikubwa nguvu ya serikali kudhibiti taarifa za mitandaoni na kuwashtaki watumiaji wa mitandao ya kijamii. Aliongeza kuwa hatua hiyo ni ukiukaji wa haki ya uhuru wa kujieleza mitandaoni na pia inakiuka viwango na sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Türkei Präsident Erdogan im Parlament
Rais wa Uturuki Recept Tayyip ErdoganPicha: Getty Images/AFP/A. Altan

Uturuki inaongoza duniani kwa maombi ya kuondolewa kwa taarifa kwa kampuni ya Twitter ikiwa na zaidi ya maombi elfu 6 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2019. Shirika la uhuru wa kujieleza, limesema kuwa zaidi ya tovuti zimefungiwa.

Tovuti ya mtandaoni ya Wikipedia ilifungiwa kwa takriban miaka mitatu kabla ya mahakama ya juu nchini Uturuki kuamua kuwa marufuku hiyo ilikiuka haki ya uhuru wa kujieleza. Watu milioni 54 kati ya milioni 83 nchini humo ni watumiaji wakakamavu wa mitandao ya kijamii.

Unaweza pia kusoma Mitandao ya Kijamii yalaumiwa kusambaa kwa Habari za Uongo

Idadi ya watu wanaounga na kupinga sheria hiyo

Utafiti uliofanywa mwezi Julai na kampuni ya kukusanya maoni ya Metropoll, ulionyesha kuwa asilimia 49.6 ya waliohojiwa hawaungi mkono sheria hiyo ambayo huenda ikazuia, kufunga ama kutoza faini kampuni za mitandao ya kijamii kuhusiana na taarifa zake. Asilimia 40.8 ya waliohojiwa walisema kuwa wataiunga mkono sheria hiyo.

Hata hivyo kampuni za mitandao ya kijamii hazikujibu mara moja kuhusiana na sheria hiyo.

Sheria hiyo ilipitishwa baada ya majadiliano makali bungeni . Sheria hiyo itachapishwa katika gazeti rasmi la serikali baada ya rais Erdogan kuiidhinisha na itaanza kutumika mwezi Oktoba.