Uturuki yaimarisha vita dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi
23 Januari 2018Operesheni hiyo iliyoanza Jumamosi wiki iliyopita, ambayo ndege za kivita za Uturuki zinavisaidia vikosi vya nchi kavu, inalenga kuwaondoa wapiganaji wa kundi la YPG, kutoka eneo la Afrin.
Uturuki inaichukulia YPG kuwa kundi la kigaidi na tawi la Syria la Chama cha Wafanyakazi cha PKK ambacho kimefanya uasi wa umwagaji damu kwa miongo mitatu dhidi ya taifa la Uturuki. Erdogan amesema hakuna kurudi nyuma "Tutaishughulikia Afrin, hakuna kurudi nyuma kutoka Afrin. Tulijadili operesheni hii na marafiki zetu Urusi, na tukakubaliana nao, na pia tulijadili hilo na majeshi mengine ya muungano na Marekani"
Lakini operesheni hiyo ni nyeti kwa sababu Marekani ililitegemea kundi la YPG kuwaondoa wapiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu – IS kutoka ngome zao za nchini Syria na wapiganaji hao wa Kikurdi sasa wanadhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Syria.
Shirika la habari la Uturuki Anadolu limesema wanajeshi wan chi kavu tayari wamevikamata vijiji 15 na maeneo mengine tangu walipoingia Syria.
Shirika la haki za binaadamu la Syria limesema jumla ya raia 22 wa Syria wamueuawa katika mashambulizi ya Utruuki na wengine wawili katika mashambulizi ya Wakurdi.
Limesema wapiganaji 54 wameuawa, wakiwemo waasi 19 wanaoungwa mkono na Uturuki, wapiganaji 26 wa Kikurdi na watu wengine tisa ambao hawajatambulika. Uturuki hata hivyo imekanusha kusababisha vifo vyovyote vya raia.
Pamoja na ugumu wa operesheni hiyo, Uturuki inakabiliwa na mazingira magumu ya kidiplomasia wakati ikitafuta kuepuka kuwatenga washirika wake na kuwachochea maadui.
Mataifa ya Magharibi yanahohia kuwa kampeni dhidi ya YPG itabadilisha lengo la kuliangamiza kundi la IS baada ya kupigwa hatua nyingi katika miezi ya karibuni
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana liliijadili operesheni hiyo ya Uturuki na mgogoro wa kiutu unaoendelea kuwa mbaya nchini Syria lakini halikulaani au kudai kusitishwa operesheni hiyo ya Uturuki.
Balozi wa Ufaransa Francois Delattre alisema baada ya mazungumzo hayo ya faragha jijini New York kuwa "anaamini wito wa kuitaka Uturuki ijizuie, ulijadiliwa wakati wa mazungumzo hayo”
Akizungumza mjini London, waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Rex Tillerson alisema ana wasiwasi kuhusu operesheni hiyo, wakati mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini akisema atajadili hali hiyo na maafisa wa Uturuki.
Lakini Erdogan alielezea kutokubaliana na madai ya Marekani kuwa aweke ratiba ya wazi, akisema operesheni hiyo itakamilika "wakati lengo lake litakapotimizwa”.
Erdogan awali aliashiria kuwa mara baada ya kuweka udhibiti mjini Afrin, Uturuki inataka kuelekea mashariki na kuwaangamiza YPG katika mji wa Manbij. Wakati huo huo, Urusi na Iran – ambazo zina majeshi yao nchini Syria na zinashirikiana na Uturuki kuhusu mchakato wa amani – pia zimeelezea wasiwasi.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Caro Robi